Thursday, 10 July 2014

ARUSHA ITAZAMWE KWA JICHO LA TATU


KATIKA historia ya Tanzania, Mkoa wa Arusha umekuwa kati ya maeneo yenye kubeba tunu nyingi za nchi hii, hususan katika sekta ya utalii na madini.

Kutokana na fursa hizo, Mkoa wa Arusha umekuwa kivutio kikubwa kwa Watanzania na raia kutoka nje, ambao humiminika kila siku kwa shughuli mbalimbali za kibiashara na kitalii na hivyo kuchangia pato la taifa.
Kwa miaka mingi, Arusha imekuwa ni sehemu tulivu kimakazi na kibiashara hususan shughuli zinazohusu madini na utalii.
Arusha ilikuwa ni mahala patulivu na salama kwa Watanzania na raia wa nchi mbalimbali, hata kubatizwa jina la ‘Geneva of Africa’, kabla ya hivi karibuni tunu hiyo kuanza kutoweka.

Arusha hivi sasa imeanza kujijengea jina baya la ‘Jiji la Mabomu’, kutokana na vitendo vinavyokithiri hivi sasa vya milipuko inayodhaniwa kuwa ni mabomu katika maeneo mbalimbali na kusababisha vifo na majeruhi.

Baadhi ya matukio ya ulipuaji mabomu mkoani Arusha ni pamoja na usiku wa kuamkia Oktoba 25 mwaka juzi, ambapo Katibu wa Bakwata mkoani humo, Abdulkarim Jonjo alijeruhiwa na bomu nyumbani kwake eneo la Esso.
Mei 5 mwaka jana, watu watatu walikufa kwenye mlipuko wa bomu katika Kanisa Katoliki la Olasiti nje kidogo ya jiji hilo, kabla ya Juni 16 bomu kulipuka kwenye mkutano wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), na kusababisha vifo.
Aprili 13 mwaka huu, mlipuko wa bomu ulitokea katika baa ya Arusha Night Park na kujeruhi watu 14 na kuua mmoja, kabla ya Julai 4 mwaka huu, Ustadhi Sudi Ally Sudi na mgeni wake aliyetambulika kwa jina la Mhaji Hussein kutoka jijini Nairobi, Kenya, kujeruhiwa na kinachosadikika kuwa ni bomu la kutupa kwa mkono wakati wakila daku nyumbani kwa ustadhi huyo.
Wakati hilo likiwa halijapoa, juzi, watu wasiojulikana walirusha kinachodaiwa bomu kwenye mgahawa ujulikanao kwa jina la Vamma karibu na viwanja vya Gymkhana na kujeruhi watu wanane, wawili kati yao vibaya.
Sisi Tanzania Daima tukiwa kama wadau wa amani na usalama, tunatoa wito kwa vyombo vya dola, kufanya kazi ya ziada kubaini matukio haya ambayo yanazidi kujijengea mtandao mkoani Arusha.
Tunasisitiza kuwa Arusha itazamwe kwa jicho la tatu ili kuirejeshea tunu yake ya ‘Geneva of Africa’.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!