WIZARA ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, imewataka wazazi kuacha tabia ya kuwageuza watoto walio chini ya umri wa miaka 18 kuwa vitega uchumi vyao.
Kauli hiyo ilitolewa jijini Dar es Salam juzi na Waziri wa wizara hiyo, Sophia Simba alipozungumza na waandishi wa habari ofisini kwake.
Alisema hivi sasa wazazi wengi wamekuwa wakiwafanya watoto wao vitega uchumi kwa kuwatafutia kazi za ndani wakiwa chini ya miaka 18, jambo ambalo ni kinyume cha sheria.
Waziri Simba alisema ni kosa kubwa kwa mzazi kumpeleka mtoto wake mwenye miaka chini ya 18 kwenda kufanya kazi za ndani wakati anatakiwa kupata elimu.
“Watoto ni taifa la kesho kwa hiyo tunapaswa kuwajengea msingi bora, ili wasije kuwa tegemezi hapo baadaye. Tuhakikishe wanapata elimu badala ya kuwageuza vitega uchumi kwa kuwatafutia kazi za ndani,” alisema.
Katika hatua nyingine, Waziri Simba aliwataka Watanzania kuacha tabia ya kuwanyanyasa wafanyakazi wa ndani kwa kuwatumikisha zaidi ya saa 12 na kuwalipa mshahara mdogo kwa kisingizio cha kula na kulala nyumbani kwa mwajiri.
No comments:
Post a Comment