KAMATI ya Ukimwi ya Halmashauri ya Kibaha Mji, mkoani Pwani, imesema bado kuna kikwazo kwa wanaume hususan walio kwenye ndoa kujitokeza kupima Virusi vya Ukimwi (VVU) na badala yake wanategemea majibu ya wake zao.
Akiwasilisha taarifa ya kamati hiyo katika kikao cha kawaida cha baraza la Madiwani wa mji wa Kibaha, Mwenyekiti wa kamati hiyo, Sloom Baghmesh, alisema ni vema wanaume nao wakabadilika na kujitokeza kwenda kupima afya zao.
Alisema kamati hiyo imekuwa ikitembelea vituo mbalimbali vya afya na kuelezewa changamoto hiyo ambayo inakwamisha jitihada za mapambano dhidi ya ugonjwa huo.
Baghmesh alibainisha kuwa sababu kubwa inayotolewa na baadhi ya wanaume hao kushindwa kujitokeza kwenda kupima VVU ni hofu na kuongeza kuwa inaonekana elimu ya kupima kwa hiari haijaeleweka vizuri kwa kundi hilo.
Kati ya Januari hadi Machi mwaka huu, jumla ya watu 2,746 wakiwamo wanaume 1,003 walijitokeza kupatiwa ushauri na kupima afya zao.
Alisema kati ya watu hao waliojitokeza 303 walikutwa na VVU wakiwamo wanawake 217 na wanaume 86.
No comments:
Post a Comment