Uongozi wa Kampuni ya Mabasi ya Sumry ya Sumbawanga, Rukwa umetoa ubani wa Sh5.5 milioni kwa familia za ndugu na jamaa waliofariki dunia kutokana na ajali ya moja ya mabasi yake iliyotokea Aprili 28 katika Kijiji cha Utaho, Wilaya ya Ikungi, Singida
Ajali hiyo ilitokea baada ya ajali ya kwanza iliyolihusisha lori na mwendesha baiskeli ambaye alipoteza maisha katika eneo hilo baada ya kugongwa na lori hilo. Wakazi hao waliogongwa walikuwa wamekusanyika kushuhudia ajali hiyo.
Kaimu Mwenyekiti wa Kijiji hicho, Hipoliti Daniel Kholani alisema rambirambi hiyo ilikabidhiwa kwa Serikali ya Kijiji na Mkuu wa Mkoa wa Singida, Dk Parseko Kone ambaye naye alichangia Sh100,000.
Kholani alisema pia Mbunge wa Singida Magharibi, Mohamed Missanga ametoa Sh600,000 na wakazi wa Tarafa ya Ihanja waishio jijini Dar es Salaam pia wamechanga Sh600,000.
“Tangu kutokea kwa ajali hiyo kijiji kimeendelea kupata idadi kubwa ya wageni kutoka sehemu mbalimbali kuja kutoa pole kwa wafiwa. Tunatarajia kufanya sala maalumu kwenye eneo la tukio kesho (leo), kuwaombea ndugu zetu.”
Kholani alisema wakazi wa kijiji hicho, Mussa Mohammed, Suku Abdallah na Ayubu Ramadhani bado wamelazwa hospitalini wakiendelea kutibiwa majeraha waliyoyapata kwenye ajali ya basi hilo ambalo bado lipo Kituo cha Polisi Ikungi
No comments:
Post a Comment