![](http://i1.ytimg.com/vi/3qQ0MCFttFc/hqdefault.jpg)
KATIKA safu yetu ya Mwana Mama, leo hii tunawaletea Saida Karoli, mwana mama mwimbaji aliyevuma kwa nyimbo zake za Maria Salome, Kaisiki, Ndombolo na Mimi Nakupenda.
Saida aliyejaliwa sauti nzuri ya kuimba na ufundi wa kupiga ngoma na kucheza, mashabiki wake walimbatiza jina la “Wanchekecha.”
Kwa wale waliofahamu lugha yake ya Kihaya, walifurahi sana maneno yake, lakini hata na wale wasiofahamu lugha ya Kihaya, waliweza kufurahia nyimbo zake ambazo utamu wake ni utamu wa muziki na wala haufuatani na maana ya maneno; Kama vile tunavyocheza na kufurahi muziki wa Nchi ya Jamhuri ya Demokrasia ya Watu wa Kongo (DRC), bila kuilewa lugha ya Lingala, ndivyo na Saida Karoli, anavyotumbuiza na kupendwa na Watanzania, Afrika ya Mashariki na Afrika yote na hata nje ya Afrika.
Ingawa umaarufu wake ulidumu kwa muda mfupi na baadaye kuzimika kama mshumaa, hakuna ubishi kwamba alikuwa mwimbaji wa kwanza Tanzania kupata umaarufu mkubwa nje na ndani ya nchi.
Ni bahati mbaya kwamba mama huyu hakuwa na elimu ya kutosha kuweza kupigania mafanikio yake; ‘mapromota’ waliomwibua ndio walioamua ‘kumzima’ baada ya kuvuna kiasi cha kutosha kutokana na jasho lake.
Kwa kiasi kikubwa mafanikio ya Saida, yameshuka, lakini akisimama juu ya jukwaa na kuimba, sauti yake bado haina mfano. Ni sauti nzuri na yakuvutia, ni sauti ya kisanii kwa vigezo vyote. Ni msanii anayeweza kuimba, kupiga ngoma na kucheza.
Ukiachia zile nyimbo zake za zamani zilizovuma, hata zile alizozitunga siku za hivi karibuni ni nyimbo nzuri na zitabaki hewani miaka mingi.
Saida hakupata elimu ya kutosha, lakini ni mtu mwenye akili nyingi na anajifunza haraka. Alipoibuka na kuiteka anga ya muziki ya Tanzania na nchi za jirani, alikuwa anafahamu lugha ya kihaya peke yake.
Hakuweza kuongea vizuri Kiswahili. Lakini baada ya muda, aliweza kuzungumza Kiswahili hata na Kingereza. Ushabiki mkubwa uliooneshwa kwa Saida, ungekuwa wa faida kubwa, kama wale wote walioonesha kumshabikia wangesaidia kujiendeleza, labda kiwango chake kingebaki juu na leo hii tungekuwa na mwimbaji wa kimataifa.
Kwa njia moja ama nyingine sote tumeshiriki kumshabikia Saida na kumsindikiza kwenye anguko lake. Hii si tabia nzuri kwenye jamii yetu ndio maana safu hii inawatafuta wanawake wenye mchango chanya katika jamii na kuandika habari zake.
Kwa njia hii tutawainua wanawake na kuwapatia moyo kuendelea kupambana na maisha. Saida alizaliwa Aprili 4, 1976, Kagera. Ni mwanamuziki wa nyimbo za asili ya Kihaya nchini.
Alipata elimu ya msingi mwisho darasa la tano tu ambapo ilibidi aache shule kutokana na kukosa msaada kutoka kwa baba yake ambaye hakuwa anaitazama sana elimu ya mtoto wake hivyo hakuweza kuendelezwa.
Saida alikulia katika Kijiji cha Rwongwe mkoani Kagera. Kutokana na mila za ukoo wake wasichana walikuwa hawaruhusiwi kushiriki katika shughuli za muziki.
Hata hivyo kwa vile mama yake alikuwa na kipaji cha muziki alimpa moyo na kumfundisha masuala mbalimbali ya muziki.
Akiwa na miaka 20 mama yake mzazi alifariki dunia lakini Saida aliendelea kujijengea kipaji chake cha uimbaji na upigaji ngoma.
Alikuwa akizunguka kijiji hadi kingine akipiga ngoma na kucheza na wakati mwingine akiambulia chupa ya pombe za kienyeji. Hakuweza kupata mafanikio makubwa kwa kuimba na kucheza kule vijijini.
Pamoja na ukweli kwamba aliimba vizuri, lakini uwimbaji wake kwa wakati ule haukuweza kumletea kipato.
Kukua kwake kimuziki
Kipaji cha usanii wa muziki kwa Saida kilijitokeza ghafla baada ya kujikuta akichukuliwa na kudhaminiwa na FM Productions Ltd waliokuwa mkoani Kagera wakitafuta wasanii wenye vipaji kwa ajili ya kuwaendeleza.
FM ilimchukua Saida wiki tatu tu kurekodi wimbo wake wa kwanza na kuishitua Dar es Salaam na nchi za jirani za Afrika Mashariki. Albamu yake ya kwanza ilizinduliwa Septemba 2 2001.
Albamu hiyo ilipata mafanikio na kupata umaarufu mkubwa sana kwa kuwa albamu hiyo ilikuwa na vionjo vingi vya kabila la Kihaya.
Albamu hiyo ilijulikana kama Maria Salome. Japokuwa mashabiki wake waliibatiza jina la ‘Chambua kama Karanga’ kutokana na maneno aliokuwa anaimba katika nyimbo ya Maria Salome nyimbo iliobeba jina la albamu.
Albamu hiyo ilifuatiwa na ziara kubwa alizokuwa anafanya katika nchi za jirani kama vile Burundi, Rwanda, Uganda na Kenya ambapo alipata mafanikio makubwa na kujikuta akibatizwa na kupewa jina la malkia wa nyimbo za asili.
Mara tu Saida kutoa albamu yake, wimbo wa Maria Salome ulipanda chati katika Kumi bora za redio kadhaa nchini na kufikia namba moja ikishikilia nafasi hiyo kwa wiki sita mfululizo.
Nyimbo zingine zilizotamba katika albamu hiyo ni pamoja na Kaisiki na Ndombolo.
Baada ya miezi mitatu tu tangu kutoa albamu hiyo, Karoli alipata mwaliko wa kuimba Uganda akialikwa na Kabaka wa Buganda katika sherehe ya kiutamaduni kama mmojawapo wa mwanamuziki aliyefanikiwa Afrika na kujulikana sana Uganda na pia kumfanya kuwa mwanamuziki wa mwaka katika sherehe ile Uganda.
Kujulikana kwake kwa kasi kulisababishwa na matumizi ya lugha ya Kihaya, lugha inayofanana zaidi na lugha ya Kiganda inayotumika na Waganda wengi, sauti nyororo na ya kuvutia na vionjo kibao vya kuvutia vya kijadi katika nyimbo zake.
Juni 2003 Saida akatoa albamu nyingine nzuri iliyokwenda kwa jina la Mapenzi Kizunguzungu na kuweza kuteka soko la muziki tena kwa mara ya pili kutokana na vionjo kama vya awali vya kijadi.
Hata hivyo Saida ametoa shukrani zake za dhati kwa Mkurugenzi Mkuu wa FM Productions LTD, Felician Mutta kwa kuona kipaji chake na kumpandisha chati kama mojawapo wa wanamuziki maarufu chini Tanzania.
Mutta alisema nia yake kwa msanii huyo ni kuona Saida anajulikana na kushika cha katika bara zima la Afrika na kuweza kufanya ziara za kimuziki nchi nyingi tu duniani.
Kutokana na uwezo alionao na kipaji katika masuala ya muziki ni rahisi kugundua kuwa mwanamuziki huyo ana kiwango cha kuweza kupata mashabiki wa muziki wake mbali na Tanzania na Afrika ya Mashariki tu, bali hata nje ya Afrika.
Nyimbo zake ni pamoja na Maria Salome, Kaisiki, Ndombolo na Mimi Nakupenda.
Huyo ndiye Saida Karoli, msanii mwenye kipaji kikubwa ambacho kikiendelezwa, taifa litakuwa na linajivunia kwenye nyanja hizi za muziki
No comments:
Post a Comment