Monday 26 May 2014

RAIS KIKWETE ATUMA SALAM ZA RAMBIRAMBI KUFUATIA KIFO CHA MWANAHABARI MAXIMILIAN NGUBE

Marehemu Maximilian John Ngube enzi za uhai wake


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho
Kikwete amemtumia salamu za rambirambi Waziri wa Habari Mheshimiwa
Dkt.Fenella Mukangara kufuatia kifo cha Mpiga picha wa kituo cha television cha  Mlimani, Ndugu Maximilian John kilichotokea alfajiri ya kuamkia leo tarehe 24  Mei,2014.
“Nimepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za kifo cha Bwana Maximilian
kilichotokana na maradhi ya Moyo, Sukari na Shinikizo la damu. Kifo hicho ni pigo  na pengo kubwa kwa tasnia ya habari hapa nchini,”Amesema Rais Kikwete katika  salamu hizo.
“Bw. Maximilian atakumbukwa kwa uchapakazi wake na uhodori katika kazi zake  siku zote. Kifo ni maandiko ya Mwenyezi Mungu hivyo hatuna budi kumshukuru kwa  yote.
“Nakutumia salamu zangu za dhati kuomboleza msiba huu. Aidha, kupitia kwako,  naitumia familia ya Ndugu Maximilian, pole za dhati ya moyo wangu kwa kuondokewa  na mzazi na mhimili wa familia. Aidha, salamu hizi ziwafikie pia wanahabari wote,  wafanyakazi wenzake, ndugu, jamaa na marafiki wa marehemu. Nakuomba uwajulishe  kuwa naelewa machungu yao katika kipindi hiki na nawaombea subira na uvumilivu.

Ninaungana nao kumwomba Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema, aiweke peponi  roho ya marehemu. Amen,” amesema Rais katika salamu hizo.

Ndugu Maximilian John ameacha mke na watoto wanne.

Imetolewa na;
Premi Kibanga,
Mwandishi wa Habari wa Rais Msaidizi,
Ikulu – Dar es Salaam.

24 Mei,2014

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!