Friday, 23 May 2014

MAMA ALIOJIFUNGUA MAPACHA WANNE AOMBA MSAADA KUTOKANA NA UGUMU WA MAISHA



Mkazi wa Kunduchi Beach Manispaa ya Kinondoni jijini Dar es Salaam, Riziki Daudi (22), akiwa amewapakata watoto wake wanne aliojifungua kwa upasuaji wiki iliyopita katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH). PICHA:OMAR FUNGO.


Mkazi wa Kunduchi Beach Manispaa ya Kinondoni jijini Dar es Salaam, Riziki Daudi (22), amejifungua watoto wanne ambao ni njiti katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) huku akiomba msaada kutokana na ugumu wa maisha.

Akizungumza na NIPASHE hospitalini hapo jijini Dar es Salaam jana, Riziki alisema kuwa alijifungua watoto hao Jumapili iliyopita ambao wawili ni wa kike na wawili wa kiume kwa njia ya upasuaji.

Aliongeza kuwa kutokana na maisha kuwa magumu, anaomba wasamaria wema wamsaidie ili aweze kuwalea watoto hao kwa maelezo kwamba mzazi mwenzake hana shughuli maalumu ya uhakika ya kuingiza kipato cha kuweza kumudu gharama za kuwalea watoto hao.

Riziki alieleza kuwa watoto hao wamezaliwa kabla ya muda na kwamba wana miezi saba.

Alisema kuwa madaktari waliamua kumfanyia upasuaji baada ya kubaini kuwa anasumbuliwa sana na kifafa cha mimba, hali ambayo ingeliweza kuhatarisha maisha yake pamoja na ya watoto hao.

“Huu ni uzazi wangu wa kwanza, lakini tatizo ni kwamba ujauzito huu umekuwa ukinisumbua sana hasa kifafa cha mimba, ambacho kilikuwa kinasababisha nipoteze fahamu mara kwa mara, jambo lililosababisha madaktari waamue kunifanyia upasuaji kabla ya ujauzito kufikisha umri wake wa kawaida yaani miezi 9 ili kuyaokoa maisha yangu pamoja na ya watoto wangu,” alisema Rikizi.

Riziki aliyeonekana kuwa na uchovu, alisema kuwa watoto hao wanaendelea vizuri ingawa mmoja ambaye ni wa mwisho hali yake haiko vizuri sana, na kwamba walizaliwa wote wakiwa na uzito sawa wa kilo moja moja.

Akizungumzia hali yake, alisema kuwa bado anaumwa na anasikia maumivu, uchovu, hana nguvu pamoja na kizunguzungu, hivyo bado anahitaji matibabu zaidi ili afya yake irejee katika hali yake ya kawaida.

“Kwa kweli bado ninaumwa, nasikia maumivu makali kwenye mshono, uchovu, sina nguvu na ninasikia kizunguzungu, hivyo bado ninahitaji matibabu zaidi ili niweze kurudia kwenye hali yangu ya kawaida.

Alieleza kuwa kwa sasa anasaidiwa na mama zake wadogo, ambao hata hivyo, hawana uwezo wa kumsaidia kuwatunza watoto hao ambao wanahitaji uangalizi maalum ili waweze kukua wakiwa na afya nzuri kama watoto wengine.

Riziki amewaomba wasamaria wema kumsaidia nepi, nguo, fedha, chakula na misaada mingine kwa ajili ya kuwahudumia watoto hao.

Watoto hao wanatunzwa kwenye wodi maalum iliyopo kwenye jengo la wazazi la MNH, chini ya uangalizi wa wauguzi.

Aliwaomba wasamaria wema ambao watakuwa wameguswa na tatizo lake kuwasiliana naye kwa namba za simu 0783717648 ya Hadija Abeid, au 0717365040 ya Thuwaiba Mohammed au 0788 711458 ya Daudi Haji.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!