Friday 30 May 2014

JAJI WA PILI AMWAGA MANYANGA KESI YA MAUAJI YA JENGO LILILOPOROMOKA JIJINI

.
 Jaji Raziah Sheikh aliyekuwa amepangwa kusikiliza maombi ya washtakiwa wa kesi ya mauaji ya jengo lililoporomoka katika Mtaa wa Indira Gandhi, amebwaga manyanga kuendelea kuisikiliza kesi hiyo.
Katika maombi hayo, washtakiwa hao wanaiomba mahakama kuu ipitie uamuzi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wa kuwanyima dhamana bila kupewa haki ya kusikilizwa ili kujiridhisha na usahihi na uhalali wa uamuzi huo uliotolewa Machi 12, 2014.
Pia wanaiomba mahakama hiyo itafakari na kupitia hati ya mashtaka waliyofunguliwa na mjibu maombi (Jamhuri), ya kubadilishiwa mashtaka kutoka mashtaka ya kuua bila kukusudia na kuwa ya kuua kwa kukusudia, ambayo ilikubaliwa na Mahakama ya Kisutu, wanayodai ni kinyume cha sheria.
Maombi mengine ni Mahakama Kuu ipitie amri zilizotolewa na Mahakama ya Kisutu kukubali mashtaka mapya bila mjibu maombi kuijulisha Mahakama mazingira yaliyosababisha kuibuka kwa mashtaka hayo mapya au kuwapa waombaji (washtakiwa) nafasi ya kusikilizwa kwa mujibu wa sheria.
Washtakiwa hao pia wanaiomba Mahakama Kuu kupitia amri ya Mahakama ya Kisutu kuwafutia dhamana bila haki ya kusikilizwa, na pia wanaiomba Mahakama itupilie mbali hati ya mashtaka mapya ya kuua kwa makusudi badala ya kuua bila kukusudia.
Maombi hayo yalitarajiwa kuanza kusikilizwa jana, lakini Jaji Sheikh alitangaza kujitoa katika usikilizwaji wa maombi hayo .
Badala yake aliamuru jalada la kesi hiyo lirejeshwe kwa Jaji Mfawidhi ili lipangiwe jaji mwingine wa kusikiliza maombi hayo na kupanga shauri hilo litajwe Juni 2, 2014, mahakamani hapo
MWANANCHI.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!