Thursday 1 May 2014

HABARI ZAIDI JUU YA WATOTO WATATU WALIOFARIKI NDANI YA SWIMMING POOL WAKIOGELEA!

KUFUATIA vifo vya watoto watatu waliokufa kwa pamoja ndani ya bwawa la kuogelea ‘swimming pool’ kwenye Hoteli ya Landmark, Mbezi Beach jijini Dar, undani  wa vifo hivyo umejulikana, Amani lina kisa kamili.
Mmoja kati ya marehemu aliyepatwa na janga hilo.
CHANZO
Kwa mujibu wa chanzo chetu, watoto walionusurika kufa ambao  walikuwa wakisherehekea siku ya kuzaliwa ya mwenzao ‘bethidei’ aliyejulikana kwa jina la Derrick Mboka, waliwaona marehemu wakielea kwenye maji ya bwawa hilo walilosema kuwa ni la kuogelea watu wazima.


Chanzo kiliendelea kuweka wazi kwamba baada ya kuwaona wenzao wakielea, watoto hao walipiga kelele jambo lililowashtua walinzi wa hoteli hiyo upande wa bwawa ambao walifika haraka kuwatoa marehemu wakiwa tayari wameshafariki dunia huku mtoto mmoja akihangaika kujiokoa.
Wanafunzi wakiomboleza kifo cha mwenzao.
“Unajua wale watoto sijui nisemeje? Waliingia mle kwenye bwawa, inaonekana walizama, hakuna aliyeweza kuja juu, maji yaliwazidi. Walipokata roho ndipo miili ikaibuka na kuelea, ndipo wenzao wakapiga kelele,” kilisema chanzo kwa masikitiko makubwa.
UZEMBE WATAJWA
Habari zaidi zinadai kuwa sababu kubwa iliyosababisha vifo vya watoto wote watatu ni uzembe uliofanywa na walinzi wa bwawa hilo ambao walidaiwa kutokuwa makini kuwadhibiti watoto wengi waliokuwa wakiogelea karibu na bwawa la watu wazima kiasi cha kutoka na kuingia huko.
Mmoja kati ya waombolezaji akilia kwa uchungu.
MAMA WA MTOTO MWENYE BETHIDEI ATUPIWA LAWAMA
Uzembe mwingine ulitajwa kufanywa na mama wa mtoto aliyekuwa akisherehekea siku yake ya kuzaliwa aliyetajwa kwa jina la Anita Mboka kwa kuwachukua watoto wasio wake na kuondoka nao bila kutoa taarifa kwa wazazi wao japo kuwa mama wa marehemu Janeth Zakaria (9), Devotha Mbutwa alikiri kupokea taarifa kuwa mwanaye anakwenda kwenye bethidei ya mwenzake beach (baharini).
Inadaiwa mama huyo alipinga mwanaye kwenda kuogelea baharini, lakini alipoambiwa ni hotelini alikubali bila kujua kuwa nako walikuwa wakienda kupiga mbizi kwenye bwawa na baadaye kupewa taarifa za kifo chake. Marehemu alizikwa jana, Iringa Vijijini.
TAARIFA ZA MTOTO WA PILI
Kwa upande wao, ndugu wa karibu wa marehemu Ndimbumi Bahati (9) walisema hawakupata taarifa yoyote kuhusiana na mzazi huyo kumchukua mtoto huyo, wakadai siku ya tukio, marehemu alipelekwa na baba yake kula chipsi jirani na alipomaliza, baba aliondoka akimuahidi kuwa atakaporejea angemchukua kumpeleka matembezini, lakini jioni akapata taarifa amefariki dunia.
Marehemu alizikwa jana jijini Mbeya.

KUHUSU MTOTO WA TATU
Nao ndugu wa mtoto marehemu Eva Nicholaus (11) hawakupatikana mara moja kwa kuwa hadi gazeti hili linaelekea mtamboni hakukuwa na msemaji rasmi wa familia hiyo ambayo  msiba wake ulikuwa Kijitonyama-Mpakani, Dar. Alizikwa jana Makaburi ya Sinza jijini Dar.
WAZAZI WAVIPOKEA VIFO KWA MTAZAMO TOFAUTI
Inadaiwa baada ya vifo vya watoto hao wa mtaa mmoja, kuna wazazi  walivipokea vifo hivyo kwa mtazamo tofauti ambapo kwa mujibu wa ndugu wa karibu wa familia ya Ndimbumi, baba wa mtoto huyo, Bahati Sisala alikuwa amechanganyikiwa kiasi cha kupoteza fahamu kwa siku nzima.
Naye mama mzazi wa mtoto Janeth, Devotha yeye alionekana kuzidi kudhoofu hali yake kwa kuwa alizipokea taarifa za kifo cha mwanaye akiwa anaumwa (ugonjwa haikujulikana).
KIJITONYAMA YAZIZIMA
Waandishi wetu walishuhudia wakazi wa Kijitonyama mahali walipokuwa wakiishi watoto hao wakiwa katika majonzi makubwa ambapo umati uligawanyika kuaga watoto hao.
Msiba wa marehemu Ndimbumi uliagwa nyumbani Kijitonyama huku mwili wa mtoto Janeth ukiagwa katika Hospitali ya Mkoa Kutabibu Kinondoni, Mwananyamala kabla ya miili hiyo kusafirishwa mmoja kuelekea Mbeya na mwingine mkoani Iringa.
WANAFUNZI WAMLILIA MWENZAO MSIBANI
Wanafunzi wa Shule ya Msingi Kijitonyama ambao walikuwa wakisoma na Ndimbumi walifika katika msiba huo na kusikitisha waombolezaji waliohudhuria msibani hapo baada ya kuangua vilio jambo lililoongeza simanzi. Marehemu alikuwa akisoma darasa la nne.

MWENYEKITI, AFISA ELIMU NA KIONGOZI WA DINI WANENA
Kwa upande mwingine Mwenyekiti wa Mtaa wa Kijitonyama, Alhaus Magoha alisema amesikitishwa sana na vifo hivyo vilivyotokea ndani ya mtaa wake na kuongeza kuwa hilo ni pigo kubwa.
Naye Afisa Elimu wa Kijitonyama, Alexandrina Kahando na Katekista wa Kanisa Katoliki Parokia ya Mtakatifu Maximilian Kolbe, Mwenge jijini Dar, John Adolf walifika msibani hapo kuwafariji wazazi wa mtoto Ndimbumi ambao walikuwa wameishiwa nguvu kutokana na kumpoteza mtoto wao mpendwa.
HOTELI YAGHARAMIA USAFIRI
Habari zilizopatikana wakati gazeti hili linakwenda mitamboni zilisema kuwa, uongozi wa Hoteli ya Landmark ndiyo uliojitolea kubeba jukumu la kuisafirisha miili ya Ndimbumi na Janet.
Juzi waandishi wetu walifika kwenye hoteli hiyo kwa lengo ka kuzungumza na uongozi lakini waliambiwa kuwa viongozi wote walikuwa kwenye vikao.
CHANZO: GPL

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!