Wednesday, 7 May 2014

DAMU INAPATIKANA BURE LAKINI.........

Siku za hivi karibuni Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii imekuwa ikitoa matangazo katika televisheni na redio kuwa damu inatolewa bure katika hospitali zote na vituo vya afya.
Matangazo hayo yanamtaka mtu yoyote kutoa taarifa iwapo muuguzi atamwambia damu haipo au amuuzie. Pengine hilo huwa gumu kwa raia kutokana na ukweli kwamba unapokuwa na mgonjwa aliyefikia hatua ya kuhitaji damu, hawezi kukumbuka kuwa kuna taasisi kama Takukuru au tangazo lililotolewa na wizara.
Hata hivyo matukio ya wagonjwa au ndugu zao kuambiwa watafute watu wa kuchangia damu, hitaji la kufanya hivyo ni jambo la kawaida. Ni utamaduni ambao Watanzania wameuzoea na pengine kuuchukulia kama utaratibu kwa mgonjwa anapotakiwa kuongezewa damu.
Mkurugenzi wa Damu Salama, Dk Festo Nkya anasema kuna upungufu wa damu nchini ambao ni matokeo ya sababu mbalimbali ikiwemo maradhi na uoga wa watu kuchangia.
Anasema kuna upungufu wa damu unaokaribia asilimia 70 ambazo ni sharti zitolewe na ndugu au marafiki wa mgonjwa inapotokea benki ya hospitali husika imeishiwa akiba iliyonayo, jambo ambalo hutokea mara nyingi.
Mahitaji ya damu kwa mwaka ni chupa 450,000. Kwa mwaka jana Mpango wa Damu Salama ulikuwa na lengo la angalau kukusanya chupa 140, 000 au hata kufikia nusu ya mahitaji.
Anasema ingawa damu inayokusanywa na mpango wa taifa, husambazwa bure katika hospitali na vituo vya afya, matumizi yake hutegemea mapendekezo yaliyowekwa. Asilimia 50 hutengwa kwa ajili ya watoto wakati asilimia 30 huwa kwa ajili ya akina mama na asilimia 15 kwa ajili ya ajali, huku tano zikitumika kwa matumizi mengineyo.
Dk Nkya anasema benki ya damu inakabiliwa na changamoto hiyo kwa kuwa pamoja na kukusanya damu nyingi, hulazimika kuzimwaga zile zinazogundulika kuwa na maradhi.
Anasema maambukizi ya Ukimwi yamepungua kwa kiasi kikubwa ukilinganisha na wakati mpango huo unaanzishwa.
“Hapo awali, wakati mpango umeanza na maambukizi ya Ukimwi yalikuwa juu, watu saba kati ya wachangiaji 100 walikuwa wanakutwa na maambukizi lakini idadi hiyo imeshuka mpaka mtu mmoja  sasa hivi,” anasema.
Anaongeza kuwa benki hiyo inakabiliwa na changamoto kuu ya homa ya ini ambayo huwalazimisha kumwaga asilimia tano ya damu wanayokusanya.
Dk Festo Nkya, licha ya kubainisha kupanda kwa takwimu za homa ya ini  na maambukizi ya virusi vyaUkimwi kupungua, anazitaja dalili kuu kuwa ni homa kali, manjano katika ulimi, ngozi na macho na pia kutapika sana.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!