Tuesday 27 May 2014

BABA,WALEZI WA MOROGORO WAPANDISHWA KIZIMBANI


BABA mzazi pamoja na walezi wa mtoto anayedaiwa kufichwa kwenye boksi kwa takribani miaka mitatu, wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi mjini Morogoro na kusomewa mashitaka ya kula njama na kufanya ukatili dhidi ya mtoto huyo.


Rashid Mvungi (47), mkazi wa Lukobe na mtumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro, ambaye ni baba wa mtoto huyo pamoja na wanandoa Mariamu Said (38) na mumewe, Mtonga Omar (30) walifikishwa mahakamani jana.



Mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Mary Moyo, Wakili wa Serikali, Sunday Hyera kwa kushirikiana na Mwendesha Mashitaka wa polisi, Anganile Msiani walidai washitakiwa walitenda makosa hayo kati ya Desemba mwaka 2010 na Mei mwaka huu katika eneo la Kiwanja cha Ndege, mjini Morogoro.

Walidai katika kipindi hicho, washitakiwa wakiwa walezi wa mtoto huyo, walimfanyia ukatili wa kumtelekeza na kumpa malezi akiwa ndani ya boksi na hivyo kumsababishia magonjwa. Walitaja maradhi yaliyomkumba mtoto huyo akiwa ndani ya boksi pamoja na utapiamlo, maumivu ya kifua na mvunjiko wa mifupa katika maeneo ya mikono na miguu.

Mawakili hao walidai upelelezi wa kesi hiyo umekamilika na kuiomba mahakama kutaja tarehe ya kuanza kusikilizwa.

Wakili wa Serikali, Hyera alidai mahakamani kwamba upande wa Jamhuri hauna kipingamizi kuhusu dhamana kwa washtakiwa.

Hakimu Moyo alisema dhamana kwa washitakiwa iko wazi ,lakini kwa masharti ya kila mmoja kuwa na wadhamini wawili watakaosaini bondi ya Sh milioni tano kila mmoja.

Alisema sharti lingine ni kwa wadhamini kuwa na barua kutoka kwa waajiri wa kuaminika au serikali za mitaa.

Washtakiwa walishindwa kutimiza masharti hayo, hatua iliyowafanya warejeshwe rumande. Kesi hiyo imeahirishwa hadi Juni 9 mwaka huu kwa ajili ya usikilizaji wa awali

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!