Sunday 25 May 2014

ALIYEKUWA KATIBU WA KARDINALI WA KWANZA MWAFRIKA, MONSINYORI BAMANYISA AFARIKI DUNIA..




Aliyekuwa Katibu wa Kardinali wa kwanza Mwafrika, Mwadhama Laurean Rugambwa, Monsinyori Justinian Bamanyisa amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 88.

Bamanyisa alifariki dunia juzi saa 5 usiku katika Hospitali ya Kagondo, mkoani Kagera alikokuwa amelazwa kwa takriban wiki mbili kutokana na ugonjwa wa saratani.
Askofu Msaidizi wa Jimbo Katoliki la Bukoba, Methodius Kilaini alithibitisha kifo hicho jana, akisema kimeacha masikitiko makubwa kwa kuwa Monsinyori Bamanyisa alikuwa mtumishi wa kanisa wa muda mrefu na kipenzi cha watu wa rika zote.
“Alikuwa mpole, mchangamfu na kwa kweli alikuwa mtu wa pekee. Alikuwa akitaniana na kila mtu, yaani watu wa kila rika,” alisema Askofu Kilaini.
Alisema atakumbukwa kwa mengi aliyofanya wakati wa uhai wake hasa ukizingatia kuwa alikuwa mtu ambaye alijitolea kwa kiasi kikubwa kwa ajili ya kusaidia wengine.
Askofu Kilaini alisema katika siku za karibuni na hasa kutokana na uzee, afya ya padri huyo imekuwa ikitetereka, lakini safari hii ameugua kwa muda usiozidi wiki mbili.
Mazishi ya Mabanyisa, mzaliwa wa Kijiji cha Irogelo, Parokia ya Rutabo, yatafanyika kesho katika makaburi ya mapadri yaliyopo Parokia ya Rubya.
Utumishi wake
Baada ya kufanya kazi na Rugambwa wakati huo akiwa askofu wa Bukoba hadi mwaka 1960 alipohamishiwa Dar es Salaam, Padri Bamanyisa aliendelea kuwa katibu wa askofu aliyefuatia, Gervas Nkalanga.
Hata baada ya Askofu Nkalanga kustaafu, aliendelea kuwa katibu wa askofu aliyeafuata, Nestory Timanywa na baadaye akateuliwa kuwa msaidizi wa askofu huyo kwa miaka 13 hadi mwaka 1988.
“Ameshika nafasi hiyo kwa kipindi kirefu katika nyakati tofauti, tutaendelea kumkumbuka,” aliongeza.
Baada ya utumishi huo, Monsinyori Bamanyisa alihamishiwa katika Parokia ya Ichwandimi na kuwa mkuu wake na baadaye alikwenda kuanzisha Parokia mpya ya Igoma hadi alipohamishiwa katika Kituo cha Kajunguti kama mlezi
MWANANCHI.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!