Friday 4 April 2014

ZANZIBAR WAKATAA SHIRIKISHO, BARA WAKACHA!

Hamad Rashid Mohamed


Wajumbe  wa Bunge Maalumu la Katiba wameanza kupitia Rasimu ya Katiba katika kamati na kuamua kwa kura baadhi ya mambo yaliyomo huku ibara sita zikikubaliwa na tatu zikikataliwa ikiwamo neno shirikisho. 
Kamati Na 5 inayoongozwa na Hamad Rashid Mohamed, imejadili sura ya Kwanza na ibara zake tisa na kufanya maamuzi kwa kura za wazi na siri.
 
Akizungumza na waandishi wa habari, Rashid alisema Kamati yake ilijadili kujadili Sura ya Kwanza na ibara zake tisa na kuwa  ibara tatu zilikataliwa ikiwamo ya shirikisho kwa wajumbe kutoka Zanzibar na sita kukubaliwa.
 
Alisema wajumbe walipewa uhuru wa kuchangia na 35 walichangia na kuruhusiwa kufanya maboresho na mabadiliko katika kila ibara au kifungu kidogo cha ibara.
 
Alisema wajumbe 38 kwa kikundi au mmoja mmoja walifanya mabadiliko ya Rasimu hiyo na kuwa baada ya kusikiliza hoja zao waliandaa bango kitita, na hatimaye kila mjumbe ambaye ametoa hoja yake kuhakikisha kwanza ameridhika kwamba yameandikwa sawa sawa maoni yake na pia alipewa nafasi ya kuwashawishi wajumbe wengine wakubaliane na hoja yake.
 
KURA

Kwa mujibu wa kanuni ya 36 (2) inayosema mapendekezo ya marekebisho, maboresho na mabadiliko yaliyowasilishwa kwa mujibu wa fasiri ya (1) yatapigiwa kura na kupitishwa kwa kuungwa mkono kwa wingi wa theluthi mbili ya idadi ya wajumbe kutoka Tanzania Bara na theluthi mbili ya idadi ya wajumbe wote kutoka Tanzania Zanzibar.
 
Fasiri (2) inasema pale ambapo  mapendekezo ya marekebisho, maboresho au mabadiliko  yatakubaliwa, ibara inayohusika ya Rasimu ya Katiba itahesabiwa kuwa imepitishwa pamoja na mabadiliko yake.
 
Kwa mujibu wa Rasimu, Ibara ya kwanza inasema Jamhuri ya Muungano ni nchi na shirikisho ambalo lina mamlaka kamili ambalo limetokana na muungano wa nchi mbili za Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya watu wa Zanzibar.
 
Alisema upande wa Bara ulikosa theluthi mbili ya kukataliwa au kukubaliwa kwa kuwa wajumbe wengi wa Bara hawakuwapo. Kwa upande wa Zanzibar theluthi mbili ilipatikana ya kukataa shirikisho.
 
 Aidha, Ibara 1 (2)  pande zote mbili zimekataa kwa thuluthi mbili. Ibara hiyo inasema Jamhuri ya muungano ni shirikisho la kidemokrasia linalofuata mfumo wa vyama vingi vya siasa, usawa wa binadamu, kujitegemea, utawala wa sheria, kuheshimu haki za binadamu na lisilofungamana na dini. 

Alisema ibara ya pili, ilikosa theluthi mbili pande zote mbili na kukataliwa, ibara hiyo inasema eneo la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni eneo lote la Tanganyika likijumuisha sehemu yake ya bahari, na eneo lote la Zanzibar likijumuisha sehemu yake ya bahari.  

Ibara ya tatu, ilipata theluthi mbili kwa kukubaliwa pande zote mbili, Ibara hiyo inatamka kuwa alama za taifa zitakuwa ni Bendera ya Taifa, Wimbo wa Taifa na Nembo ya Taifa kama zitakavyoainishwa katika sheria za nchi.
 
Ibara ya nne ilipata theluthi mbili ya kukubaliwa pande zote mbili. Ibara hiyo inatamka kuwa lugha ya Taifa ya Jamhuri ya Muungano  ni Kiswahili.
 
Ibara ya tano ilikosa theluthi mbili za kukataliwa kwa pande zote. Ibara hiyo inasema Jamhuri ya Muungano itazingatia na kuenzi Tunu za Taifa zikiwamo, utu, uzalendo, uadilifu, umoja, uwazi, uwajibikaji, na lugha ya taifa.
 
 Ibara ya sita ilipata theluthi mbili ya kukubaliwa pande zote mbili. Ibara hiyo inaeleza kuwa Jamhuri ya Muungano ni nchi inayofuata misingi ya demokrasia inayozingatia haki ya kijamii na kwa hiyo wananchi ndiyo msingi wa mamlaka yote, na serikali itapata mamlaka na madaraka kutoka kwa wananchi.
 
Ibara ya saba ilikosa theluthi mbili ya kukubaliwa pande zote mbili, ambayo inasema Muundo wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano, na vyombo vyake katika uendeshaji na utekelezaji wa shughuli zake, utazingatia azma ya kukuza umoja wa kitaifa na kudumisha heshima ya taifa.
 
Ibara ya nane ilipata theluthi mbili ya kukubaliwa pande zote mbili, ambayo inasema Katiba hii ni sheria kuu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuzingatia masharti ya Katiba hii na Ibara ya tisa ilipata theluthi mbili ya kukubaliwa, ambayo inasema mtu au kikundi cha watu hakitachukua au kushikilia mamlaka ya nchi isipokuwa kwa mujibu wa Katiba hii.
 
“Hapa inaonyesha kuwa si vyama wala nini, bali watu wenyewe wamefika mahala wakasema hili tunalikubali na hili hatulikubali,” alisema.
 
Alisema asilimia 90 ya kura zilizopigwa kulikuwa na wajumbe watano au sita ndiyo waliokuwa wakipiga kura za siri. 

“Chakusikitisha tulitumia muda mwingi kujadili sura ya wazi na siri lakini kwenye kamati tunapiga zaidi kura ya wazi, kumbe watu wengi walipenda kupiga kura ya wazi," alisema.
 
Alisema wajumbe wamejitahidi kufanya utafiti kwa kutumia nyaraka walizopewa na wenyewe wamefanya tafiti zao mbalimbali na kuhoji mkataba wa muungano kutoonekana.
 
“Kulikuwa na mazungumzo yenye uhai mkubwa kwenye kamati yetu jambo ambalo ni la faraja sana, kwa maana hiyo tunategemea kupata Katiba nzuri kama hali tuliyotoka nayo kwenye kamati ndiyo tutakayokwenda nayo bungeni Ijumaa,” alisema.
 
*Imeandaliwa na Beatrice Bandawe, Emmanuel Lengwa, Ashton Balaigwa na Jacqueline Masano, Dodoma.
 
SOURCE: NIPASHE

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!