Sunday, 13 April 2014
WATANZANIA WATEMBEA KIFUA MBELE KWA TUZO YA KIKWETE
“Tunatoa pongezi kwa Rais Kikwete kwa kutunukiwa tuzo hiyo ambayo inatuweka Watanzania juu katika masuala ya uongozi na utawala bora na sasa tunatembea vifua mbele,'' alisema Balozi wa Tanzania nchini Marekani, Liberata Mulamula katika mkutano wake na waandishi wa habari juzi jijini Washington.
Alifafanua kwamba Rais amekuwa kiongozi wa kwanza katika Afrika Mashariki kutunukiwa tuzo hiyo baada ya kupata kura nyingi zilizopigwa kupitia mitandao kufuatia shindano lililokuwa linaendeshwa na jarida la African Leadership.
Tuzo hiyo ilipokelewa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Tanzania, Bernard Membe kwa niaba ya Rais Kikwete katika hafla ambayo pia ilihudhuriwa na Balozi wa Nigeria nchini Marekani, Ade Adefuye aliyekuwa anamwakilisha Rais wa nchi yake, Goodluck Jonathan.
Jarida la African Leadership linamilikiwa na wananchi wa Nigeria na kuchapishwa jiji hapa.
Akijibu maswali katika mkutano huo, Balozi Mulamula alieleza pia kwamba ziara aliyoifanya Rais wa Marekani, Barack Obama nchini Tanzania mwaka jana imefungua milango na kuweka mazingira mazuri ya kuvutia biashara na uwekezaji.
HABARI LEO
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment