Monday 14 April 2014

KWAHERI MAALIM GURUMO!

NGULI wa muziki wa dansi nchini, Muhidin Maalim Gurumo ‘Mjomba’, amefariki dunia jana katika hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) akiwa na umri wa miaka 73.

Gurumo, mwanamuziki mwenye historia ndefu ya muziki nchini, alikuwa akisumbuliwa na maradhi ya moyo kwa muda mrefu na kumfanya astaafu muziki hivi karibuni.
Mwanamuziki huyo aliyeongoza jahazi la Msondo Ngoma kabla ya kustaafu, alifariki dunia jana majira ya saa nane mchana katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili alipokuwa amelazwa tangu juzi baada ya kuzidiwa.
Akizungumza na Tanzania Daima kwa njia ya simu, mjukuu wa marehemu, Ramadhan Shabani, alisema babu yake alizidiwa juzi na hatimaye akakimbizwa katika Hospitali ya Muhimbili hadi alipopoteza maisha jana.
Shabani alisema kuwa jana familia ilikuwa inapanga sehemu watakayompumzisha Kamanda Gurumo, lakini taarifa za awali zinasema kuwa anatarajiwa kuzikwa leo saa tisa katika makaburi ya Masaki, nyumbani kwake Kisarawe, mkoani Pwani.
“Babu anatarajiwa kuzikwa leo saa tisa katika makaburi ya Masaki au Kibada… Masaki ni kwa upande wa mama yake na Kibada baba yake. Kati ya sehemu hizo mbili tutaamua,” alisema Shabani.
Alisema kwa sasa msiba wa Kamanda Gurumo upo nyumbani kwake Makuburi Ubungo, jijini Dar es Salaam.
Kiongozi Msaidizi wa bendi ya Msondo, Totoo Ridhiwani, alisema kuwa wanamuziki wa Msondo wamepokea kwa mshituko mkubwa taarifa za kifo cha Gurumo.
Gurumo ameanza kazi ya muziki tangu miaka ya 1960 na aliimba katika bendi mbalimbali zikiwemo NUTA Jazz, Mlimani Park na safari yake ya muziki aliimaliza akiwa na Msondo Ngoma.
Gwiji huyu ndiye muasisi wa mitindo ya ‘Msondo’, ‘Sikinde’ na ‘Ndekule’ katika bendi za NUTA Jazz, Mlimani Park na Orchestra Safari Sound (OSS).
Ameacha mke, watoto sita na wajukuu wawili.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!