Friday 18 April 2014

KAZI ZA KUJITOLEA ZILIVYOMPA UBALOZI VICTORIA BECKHAM UNAIDS

AKIWA amejikita zaidi katika kazi za kujitolea na kusaidia jamii kwa kushirikiana na mumewe, David Beckham, mwanamuziki wa zamani wa kundi la ‘Spice Girls’ Victoria ‘Posh Spice’ Beckham, hatimaye ndoto yake ya siku nyingi imetimia baada ya kuteuliwa kuwa Balozi Maalumu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kudhibiti Ukimwi (UNAIDS), katika kampeni kabambe kwa watoto na vijana wanaoishi na virusi vya ukimwi.

Nia kuu ya shirika hilo la UNAIDS ni kuwafikia watu wapatao milioni 15 wanaoishi na virusi vya ugonjwa huo hatari kwa kuwapa matibabu na elimu maalumu ya kuzuia maambukizi mapya kwa asilimia 50 hadi kufikia mwaka wa 2015.
Victoria anayetimiza miaka 40 ya kuzaliwa wiki hii, amekuwa akishirikiana bega kwa bega na mume wake katika kuchangisha na kutoa michango mbalimbali kwa watu na hasa watoto wenye matatizo.
Mwaka jana walichangisha michango mingi kutoka kwa wabunifu wa nguo kwa kushirikiana na Shirika la Msalaba Mwekundu (Red Cross) huko Chelsea na kukabidhi pesa kwa wahanga wa ‘Typhoon Haiyan’.
Wakiwashirikisha watoto wao katika shughuli za kusaidia jamii, mtoto wao wa kwanza Brooklyn alikaririwa akisema kuwa hawataki kupokea asante au zawadi maalumu kutoka kwa watu au yeyote aliyefaidika na misaada wanayoitoa au kupitia kwao.
Mitindo na biashara
Victoria Caroline Adams anayejulikana pia kama ‘Posh Spice,’ alishawahi kuwa mwimbaji wa zamani wa kundi maarufu la Spice Girls.
Mama huyo mwenye watoto 4, ambaye ni mke wa nahodha wa zamani wa timu ya taifa ya Uingereza, David Beckham, mbali ya uanamuziki pia ni mbunifu wa mitindo na ni mfanyabiashara.
Katika harakati zake za kibiashara, ameshazindua lebo inayojulikana kama ‘Line of Jeans’ na ‘Rock & Republic’ na ametengeneza lebo inayojulikana ‘dVb Style.’
Akifanya kazi zake nchini Uingereza na Marekani kwa kushirikiana na Japanese Store chini ya Samantha Thevasa na Shiatzy Chen, aliweza kuzalisha mikoba ya kike na mapambo ya vito vya dhahabu.
Vilevile, mwanamama huyo ameshatunga vitabu viwili vilivyopata mauzo mazuri ambako kitabu kimoja kinazungumzia maisha yake na kingine kinatoa mwongozo wa fani ya mitindo.
Katika mafanikio mengine, Victoria ameshiriki katika ‘Dokomentari’ zinazohusiana na kazi zake yeye mwenyewe na pia katika maonyesho mbalimbali katika TV nchini Marekani.
Sherehe za kutimiza miaka 40
Akitafakari kwa kina amefanya nini katika miaka 40 ya kuzaliwa kwake, inaelezwa kwamba siku hiyo ataisherehekea akiwa na familia yake kwa mlo maalumu  katika mgahawa wa kawaida wa LA Restaurant.
Chanzo kimoja kilichoko karibu naye kimeliambia gazeti la kila siku la Mirror linalochapishwa nchini Uingereza kuwa, karamu hiyo ndogo itakuwa na kila kitu cha gharama kubwa ila tu siku yake hiyo muhimu itasherehekewa kimyakimya.
Wageni maalumu na waalikwa watakuwa ni wazazi wake watakaoruka na ndege kutokea Uingereza ili kuungana na binti yao katika sherehe hiyo itakayofanyika nchini Marekani.
Marafiki zake wa karibu wanaoandaa sherehe hiyo ni Eva Jacqueline Longoria, ambaye ni mtangazaji maarufu wa runinga nchini Marekani na mwigizaji wa filamu akishirikiana bega kwa bega na mkali wa upambaji wa nywele Kevi Paves.
Wanamuziki wenzake wa kundi la ‘Spice Girls’ kina Mel B, Geri Halliwell, Mel C na Emma Bunton hawatakuwepo katika hafla hiyo ya kuadhimisha miaka 40 ya kuzaliwa, bali meneja wake wa zamani Simon Fuller amealikwa.
Aliyoyafanya mbali na muziki
Victoria siku za nyuma alishaandaa tamasha maalumu jijini London kwa kushirikiana na Balozi Maalumu wa Michezo ya Olimpiki, Nicole Scherzinger, anayejulikana pia kwa jina la Nicole Prescovia Elikolani Valiente, ambaye ni mtunzi na mwanamuziki.
Katika tamasha hilo ambalo walimshirikisha Eva Longoria, baadhi ya mapato yalilenga katika kusaidia makundi maalumu ya kijamii.
Historia yake
Victoria alizaliwa katika Hospitali ya Princess Alexandra, huko Herlow, Essex na kuishi Goffs Oak, Hertfordshire akiwa ni mtoto wa kwanza kati ya watoto watatu wa Jacqueline Doreen na Injinia Anthony William Adams.
Victoria alijiingiza katika sanaa za maonyesho na pia kusomea dansi na mitindo akiwa katika shule ya St. Mary High School huko Cheshunt nchini Uingereza.
Aliweza kumiliki jukwaa kwa kuimba na kucheza na ilipofika mwaka 1994 alijiunga na kundi la muziki la ‘Spice Girls’ na wakati huo alikuwa akitumia  jina la Victoria Adams katika kazi zake.
Wimbo wake wa kwanza kutoka nao mwaka 1996 aliupa jina la ‘Wannabe’, ambako aliweza kufanya kazi nzuri kwa kushirikiana na wanamuziki wenzake kina Geri Halliwell, Emma Bunton, Melanie Brown na Melanie Chisholm.
Kutokana na kujituma kwa kundi hilo, liliweza kuwa namba moja la muziki linalofanya vizuri nchini Uingereza na Marekani na hapo ndipo Victoria akapewa jina la utani la ‘Posh Spice

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!