Mganga Mkuu wa Hospitali ya Mkoa wa Mtwara, Ligula, Dkt. Shaibu Maarifa (katikati) akizungumza na Timu ya Ukaguzi wa Miradi ya Maendeleo kutoka Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango ilimpotembelea Ofisini kwake. Kushoto ni viongozi wa Timu hiyo, Prof. Longinus Rutasitara (Kushoto) na Bibi Florence Mwanri (Wapili kulia).
Mganga Mkuu wa Hospitali ya Mkoa wa Mtwara, Ligula, Dkt. Shaibu Maarifa (Wapili kulia, aliyenyanyua mikono) akiwaonesha eneo litakapokuwepo Hospitali mpya ya rufaa mkoani humo wakati wa Timu ya Ukaguzi wa Miradi ya Maendeleo kutoka Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango ilipofika kujionea maendeleo ya maandalizi ya awali ya ujenzi wa hospitali hiyo.Mthamini Mkuu wa Ardhi wa Mkoa wa Mtwara, Bw. Abdallah Komba (aliyeinama) akiwaelekeza namna ya hospitali ya rufaa ya mkoa huo itakavyokuwa wakati Timu ya Ukaguzi wa Miradi ya Maendeleo kutoka Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango ilipotembelea mradi huo.Sehemu ya uzio unaozunguka eneo likalojengwa Hospitali mpya ya rufaa mkoani Mtwara.
Picha na Saidi Mkabakuli
………………………………………………………..
Na Saidi Mkabakuli
Wakazi wa mikoa ya kusini ikiwemo Mtwara, Lindi, na Ruvuma inatarajiwa kupata hospitali ya kisasa ya rufaa itakayojengwa katika eneo la Mikindani, nje kidogo ya mkoa wa Mtwara katika lengo la kuhakikisha kuwa ukuaji wa uchumi unakuwa shirikishi na kuendelea kuboresha huduma za jamii hususan na afya katika mikoa hiyo.
Hayo yamesemwa na Mganga Mkuu wa Hospitali ya Mkoa wa Mtwara, Ligula, Dkt. Shaibu Maarifa wakati akizungumza wakati wa mkutano wa pamoja na Timu ya Ukaguzi wa Miradi ya Maendeleo kutoka Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango ilipofanya ziara ya ukaguzi wa maendeleo ya katika mkoa huo.
“Mradi wa hospitali ya Rufaa ya Mtwara umelenga kutoa huduma za rufaa kwa kanda ya kusini hususan mikoa ya Mtwara, Lindi, na Ruvuma, hospitali hii itakapokamilika inategemewa kuchukua wagonjwa wa nje na ndani watakaohudumiwa kwenye vitengo mbalimbali vinavyojitosheleza kwa vifaa na wataalamu, “ alisema Dkt. Maarifa.
Kwa mujibu wa taarifa za awali mradi ulianza kutekelezwa katika mwaka wa fedha 2012/13 kwa fedha za Serikali zinazotolewa kupitia ngazi ya wizara ambapo mpaka sasa ujenzi wa uzio kuzunguka eneo hilo umekamilika.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo, mmoja wa viongozi wa timu ya ukaguzi wa miradi ya maendeleo kutoka Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango, Bibi Florence Mwanri alisema kuwa serikali inatambua umuhimu wa suala la afya kwa wakazi wa mikoa ya kusini, na akatoa wito kwa uongozi wa mkoa kuzingatia na kusimamia matumizi sahihi ya fedha za serikali katika mradi huo.
“Madhumuni ya mradi ni mazuri hivyo mkoa kupitia wizara kuweka msukumo kwa kuhakikisha mradi unakamilika na kutelezwa kwani utachangia kuboresha huduma za afya katika maeneo ya kusini na kupunguzia wananchi mzigo wa gharama kwa kufuata hospitali zilizo mbali na mikoa yao,” alisema Bibi Mwanri ambaye ni Naibu Katibu Mtendaji anayeshughulikia Huduma za Jamii na Maendeleo ya Idadi ya Watu.
Kwa mujibu wa Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano (2011/12 – 2015/16) eneo la afya ni kipaumbele cha nne cha mkakati kwa lengo la kuongeza maendeleo ya rasilimali watu na ujuzi ambapo Mpango unahimiza kuwekeza katika elimu hasa katika elimu ya juu na vyuo vya huduma za afya na uongezaji ubora na upatikanaji wa huduma hizo katika kujenga nguvu kazi itakayoleta maendeleo ya kiuchumi na kijamii nchini Tanzania.
Serikali imeaandaa Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano ukiwa na lengo la kuwa na mfumo madhubuti wa kutekeleza Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025. Lengo la Dira ni kuibadili Tanzania kuwa nchi ya uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.
No comments:
Post a Comment