Raia wawili wa Ufaransa wameuawa na kutumbukizwa katika kisima cha maji kilichomo ndani ya uwanja wa nyumba yao na watu wasiojulikana katika eneo la Shehia ya Matemwe Kaskazini, Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Habari zilizopatikana na kuthibitishwa na Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai Zanzibar (DCI), Yussuf Ilembo zinaeleza kuwa watu hao mtu na mkewe waliuawa hivi karibuni.
DCI Ilembo aliliambia gazeti hili jana kuwa tayari vikosi vya Zimamoto na Uokozi (KZU) na Polisi vimeanza kufukua kisima hicho na kwamba katika hatua ya awali wamefanikiwa kukuta mfupa wa mguu wa kushoto wa mmoja wa watu hao.
Aliwataja wazungu hao kutoka Ufaransa kuwa ni Francois Cherer Robert Daniel na Brigette Mary ambao walikuwa wakiishi kama mtu na mkewe wakiwa na mbwa wao anayeitwa Allan ambaye pia amekutwa amekufa ndani ya nyumba hiyo.
Alisema uchunguzi wa awali umeonyesha kuwa Wafaransa hao waliingia nchini kihalali mwaka 2013, na kununua nyumba kwenye ufukwe wa mwambao wa Bahari ya Hindi eneo la Matemwe na kuanza kuishi eneo hilo.
DCI Ilembo alisema polisi tayari wanawashikilia watu watatu wakazi wa Shangani katika Mjimkongwe wa Zanzibar na mmoja anayeishi katika eneo la Kilimani katika wilaya ya Mjini Unguja.
“Kuna askari wanaendelea na kazi ya kuzamia ndani ya kisima kilichomo ndani ya uzio wa nyumba hiyo, kazi bado ni kubwa na siyo ya siku moja,” alisema DCI Ilembo.
Gazeti hili limefanikiwa kufika katika eneo la nyumba hiyo na kukuta askari Polisi wanne wakilinda nyumba hiyo huku harufu kali ikitoka katika shimo la kisima.
Hata hivyo, mlinzi wa nyumba hiyo ametoweka katika mazingira ya kutatanisha na simu yake kila ikipigwa imezimwa.
Mlinzi mpya aitwaye Omar Juma ambaye amekutwa akilinda nyumba hiyo baada ya kuajiriwa na mtuhumiwa mmoja aliyekamatwa amesema alikabidhiwa kazi ya ulinzi kuanzia Januari mwaka huu na hakumkuta mtu yeyote akiishi hapo.
“Kazi yangu ni kazi za ulinzi, nimeletwa hapa na mwajiri, sijui lolote, mwajiri wangu ndiye anayejua kama kulikuwa na watu kabla au la, sina la kusema na sijui nianzie wapi,” alisema Omar.
Sheha wa Matemwe Kusini
MWANANCHI.
No comments:
Post a Comment