Tuesday 4 February 2014

RAIA 3 WA SYRIA WAKAMATWA WAKIJIANDAA KUELEKEA ROME ITALY


Raia watatu wa Syria wamekamatwa  walipokuwa wakijiandaa kusafiri kupitia uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume (AAKIA) kuelekea Rome Italy kwa kutumia ndege ya Italy yenye nambari 193253 tarehe 29/01/2014.
Raia hao ni Mamdoh ALasfar Yousuf aliezaliwa tarehe 01/08/1975 katika mji wa Hama Syria, Mohd Akram Adnan aliyezaliwa tarehe 14/01/1995 Damascus  na Bibi Razan Adnan Alkurdi aliezaliwa Damascus tarehe 01/01/1994.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Idara ya Uhamiaji Zanzibar kwa vyombo vya habari, Mamdoh Alasfar Yousuf  alikuwa na pasi ya kusafiria nambari 006011215 iliyotolewa tarehe 24/02/2011 Hama Syria na aliingia nchini kwa mara ya kwanza tarehe 21/12/2013 kupitia AAKIA  na kuondoka tarehe 29/12/2013 kwa kupitia AAKIA akiwa na pasi yake halali ya kusafiria.

Mamdoh alikamatwa AAKIA akitumia pasi ya kusafiria ya Taifa la Bulgaria yenye nambari 308991470 iliyotolewa tarehe 28/05/2010 kwa kutumia jina la kughushi ambalo ni Anastas Dimitrov Karabobov.

Mohd Akram Adnan alikuwa na pasi ya kusafiria nambari 0073573492 iliyotolewa tarehe 22/10/2012  aliingia nchini kwa mara kwanza tarehe 15/01/2014 kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Kambare Nyerere (JKNIA) akiwa na pasi yake halali ya kusafiria.

Mohd alikamatwa AAKIA akitumia pasi ya kusafiria ya   kughushi  ya Taifa la Luxembourg yenye nambari G 76CB80 iliyotolewa tarehe 14/07/2009 yenye jina la kughushi Hosam Jaber.

Taarifa hiyo imeongeza kuwa Bibi Razan Adnan Alkurdi alikuwa na pasi ya kusafiria nambari 006425707 iliyotolewa tarehe 27/08/2011 na aliingia nchini tarehe 15/012014 kupitia JKNIA.

Razan alikamatwa AAKIA akitumia pasi ya kusafiria ya kughushi ya Taifa la Sweden yenye nambari 0966629944 iliyotolewa mwezi Disemba 2004 kwa kutumia jina  la Laila Mohd.

Raia hao walizuiliwa kuondoka nchini kwa vile waligundulika kutumia pasi za kusafiria za kughushi ambalo ni kosa kwa mujibu wa sheria za Uhamiaji pamoja na sheria za kimataifa za kusafiria kifungu 31(1)(e)(g)(o).

Baada ya kuhojiwa na kufanyiwa uchunguzi wa kina na Maafisa Uhamiaji ilibainika pamoja na kuwa na hati za kusafiria za kughushi walikuwa na pasi zao halali za kusafiria pamoja na tiketi rejea walipoondokea.

Baada ya kuhojiwa raia hao walipelekwa Polisi Madema ambako walikaa kwa muda wa siku mbili na baadae wakakaa Hoteli ya Tembo siku moja na wakasafirishwa na Afisa Uhamiaji husika kupitia AAKIA.

Taarifa hiyo imebainisha kwamba kwa mujibu wa taratibu za kimataifa za usafiri zinazoongozwa na Shirika la Kimataifa la usafiri (ICAO) zinaelekeza msafiri aliegundulika kufanya makosa ya kiuhamiaji anatakiwa kurejeshwa kituo cha mwisho alichoondokea, hivyo Idara ya Uhamiaji Zanzibar iliwarejesha raia hao wa Syria Uwanja wa ndege wa Kimataifa wa JKNIA tarehe  31/01/2014 ambacho ni kituo walichoingilia nchini. Kunataarifa kuwa JKNIA wameshawarejesha raia hao wa Syria kituo walichotoka.
Uchunguzi wa awali wa tukio hilo inaonekana raia wa kigeni hasa kutoka mataifa yenye mizozo wanakimbilia nchi mbali mbali za Ulaya kwa kupitia baadhi ya nchi ikiwemo Tanzania na mara nyingi kusaidiwa na wenyeji wenye nia mbaya kama ilivyojitokeaza katika tukio hilo.
NA ZANZIBAR NEWS.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!