Mshtakiwa Makongoro Joseph Nyerere, anayekabiliwa na kesi ya mauaji ya kukusudia ya mfanyabiashara wa madini, ameiomba Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imuachie huru akakae nyumbani na watoto wake.
Mbali na Makongoro, mshtakiwa mwingine anayekabiliwa na kesi hiyo ni Mfanyabiashara, Marijan Abubakar ‘Papa Msofe’ (50) ambaye hakuwepo mahakamani na ikatolewa taarifa kuwa ni mgonjwa.
Makongoro alitoa ombi hilo jana mbele ya Hakimu Mkazi, Hellen Liwa baada ya Mwendesha Mashtaka wa Polisi, Inspekta Jackson Chidunda kudai mahakamani hapo kuwa kesi ilikuja kwa ajili ya kutajwa na upelelezi bado haujakamilika.
Chidunda aliendelea kudai kuwa jalada halisi la kesi hiyo lipo kwa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) linasomwa. Baada ya kutolewa kwa maelezo hayo, Makongoro alilalamika kuwa yeye hana kesi na kuiomba mahakama imuachie huru akakae nyumbani na watoto wake.
Mshtakiwa huyo alidai kuwa yeye alikuwa akifanya kazi halali, lakini anaambiwa kuwa ameua kisa Sh8 milioni alizokataa kuwapatia polisi baada ya wao kumtaka awape.
Kutokana na malalamiko hayo, Hakimu Liwa aliutaka upande wa mashtaka kuharakisha upelelezi na kuiahirisha kesi hiyo hadi Machi 11, 2014 ili kuangalia upelelezi kama utakuwa umeshakamilika ama la.
MWANANCHI.













No comments:
Post a Comment