Rose Kamili (MB) mwenye kofia nyekundu alipokuwa akitangaza kuwania urais 2015
MBUNGE wa Viti Maalumu mkoa wa Manyara kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema),Rose Kamili ametangaza kugombea urais katika Uchaguzi Mkuu wa 2015.
Alitangaza kuwania nafasi hiyo leo mbele ya wajumbe wa kamati ya kudumu ya bunge ya maendeleo ya jamii iliyokuwa ikitembelea shughuli mbalimbali za wizara ya maendeleo ya jamii, mjini Iringa.
Wakiwa katika Chuo cha Maendeleo ya Jamii Ruaha kilichopo Ipogolo mjini Iringa, Kamili alisema “Naitwa Rose Kamili mimi ni mbunge wa viti maalumu mkoa wa Manyara kupitia Chadema na napenda kutumia fursa hii kutangaza rasmi kwamba nitawania urais katika Uchaguzi Mkuu wa 2015.”
Baadhi wabunge wenzake wa kamati hiyo walipiga makofi huku wageni wengine waalikwa katika ziara ya wabunge hao chuoni hapo wakicheka.
Baada ya kutangaza azma yake hiyo aliketi kwenye kiti chake huku akisema anataka kudhihirisha ule msemo usemao wanawake wanaweza.
Katika hali ya utani, mwenyekiti wa kamati hiyo, Said Mtanga alisema “hata kama ukikosa, huenda ukawa first lady endapo mumeo Dk Wilbroad Slaa atapata nafasi hiyo”, kauli iliyoacha kicheko kutoka kwa wajumbe wengine.
Kamili (mwenye kofia nyekundu) akiwa na wajumbe wenzake wa kamati ya bunge ya maendeleo ya jamii katika chuo cha maendeleo ya jamii Ruaha, mjini Iringa |
Akipongeza uamuzi wa Kamili, Mbunge wa Mtera Livingstone Lusinde alisema Rose Kamili ameonesha ujasili mkubwa kutangaza nia yake hiyo.
“Ni ujasiri hasa katika kipindi hiki ambacho ndugu zetu Chadema wamemvua uongozi aliyekuwa naibu katibu mkuu wao, Zitto Kabwe wakimtuhumu kwa makosa mbalimbali,” alisema.
Aliitaja moja ya sababu iliyopelekea Kabwe apate adhabu hiyo ni kutangaza kugombea urais kupitia chama hicho wakati kuna kila aina ya dalili inayoonesha kwamba Dk Slaa atagombea urais kwa mara nyingine tena katika uchaguzi ujao.
“Narua amafanya ujasiri kutangaza mbele ya wajumbe wa kamati, wanachuo na watumishi wa chuo hiki, lakini nina wasiwasi kama yaliyompata Zitto yanaweza kunusurika kwake,” alisema.
Akitaka kunukuliwa kama Mbunge wa Kondoa Kusini, naibu Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo Juma Nkamia alisema ameshtushwa na uamuzi wa Kamili.
“Nachoweza kusema hiyo ni demokrasia, lakini kama mbunge mwenzake imenishitusha sana kwasababu katika mazingira ya kawaida inahitaji ujasiri ndani ya Chadema kutangaza kugombea urais,” alisema.
“Kila mtu anajua kwamba Rose Kamili amekuwa na mahusiano ya mume na mke wa Dk Slaa; anavyotangaza kuwania nafasi ambayo kuna kila dalili kwamba mumewe ataiwania, haogopi kufukuzwa chama?,” aliuliza.
Julai mwaka jana, Kamili anayedai kuwa ni mke wa Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Slaa alifungua kesi Mahakama Kuu Kanda ya Dar es salaam akiiomba isimamishe ndoa ya kiongozi huyo na mchumbe wake Josephine Mushumbuzi iliyokuwa ifungwe Julai 21, mwaka jana.
Katika kesi hiyo, Kamili aliiomba mahakama imuamuru pia Dk Slaa amlipe Sh Milioni 50 kama fidia ya matumizi anayofanya pasipo matunzo ya mumewe huyo.
Kwa kupitia wakili wake, Joseph Thadayo, Kamili aliiomba mahamaka hiyo imuamuru Mushumbuzi amlipe kiasi cha Sh Milioni 500 za fidia ya maumivu aliyopata kutokana na kitendo chake cha kuingilia ndoa yao.
Katika hati hiyo ya madai, mbunge huyo alidai kuwa ndoa inayotarajiwa kufungwa kati ya Dk Slaa na Mushumbuzi ni batili kwasababu kuna ndoa nyingine halali na inayoendelea kuishi kati ya Dk Slaa na Kamili iliyofungwa mwaka 1985.
Kamili anadaiwa pia kuwasilisha hati hiyo ya mashtaka kwa Mwadhama Polycarp Kaadinali Pengo akimweleza Askofu huyo wa Jimbo Katoliki la Dar es salaam kuwa moja ya Parokia za Dar es salaam zilikuwa na taarifa ya ndoa hiyo.
Nakala ya madai hayo zimeelezwa kuwasilishwa kwa Msajili wa Mahakama kuu, Msajili wa Ndoa na Askofu Mkuu wa Jimbo Katoliki la Mbulu.
Oktoba mwaka jana, mahakama hiyo ilitupilia mbali kwa gharama pingamizi lililowasilishwa mbele yake na Dk Slaa lililokuwa likiiomba mahakama iyo ifute kesi hiyo ya madai namba 4 ya mwaka 2012 iliyofunguliwa na Kamili.
CREDIT:Frank Leonard
No comments:
Post a Comment