Katika maisha ya kila siku inaweza kutokea ukapenda kufanya jambo fulani ambalo kwa wakati huo linaweza likakosa faida kwako, lakini baadaye jambo hilo ndilo likawa mkombozi wa maisha yako.
Ukweli wa maelezo hayo unathibitishwa na Faith Mwaisala, ajuza mwenye umri wa miaka 74, ambaye tangu usichana wake amekuwa akitumia muda mwingi kutengeneza bustani za maua, bila kupata faida yoyote, lakini sasa maua hayo yamekuwa ndiyo mkombozi wa maisha yake.
Pamoja na uzee wake Faith, amekuwa akiendesha maisha yake kwa biashara ya upandaji maua na kuyakodisha kwa wapambaji wa shughuli mbalimbali ikiwamo harusi, mikutano, semina, sherehe za kuzaliwa na mambo kama hayo.
Faith ambaye ni askari polisi mstaafu anasema kuwa tangu akiwa kazini, alikuwa akiyapa kipaumbele maua bila kufahamu kwamba maua hayo baadaye yatamwezesha kuendeshea maisha yake.
Anaeleza kuwa aliingia rasmi kwenye biashara ya maua mwaka 1993, baada ya kustaafu kazi na tangu hapo anaendelea na biashara hiyo licha ya umri wake kusonga mbele.
“Binafsi ninapenda maua, nilikuwa nahakikisha kila aina ya ua linapatikana nyumbani kwangu kama sehemu ya mapambo. Sikufahamu kama siku moja yanaweza kuwa biashara, lakini baada ya kustaafu kazi nilianza kuona manufaa ya maua,”anasema Faith.
Kwa mujibu wa Faith bei ya maua yake hutegemea wakati na msimu wa shughuli nyingi ua moja hukodishwa kwa kati ya Sh1,000 hadi 1500 na endapo mteja atahitaji kununua atalipa Sh40,000 kwa maua yanayotumika kupambia katika kumbi za sherehe.
Anasema kuwa licha ya umri wake kuwa mkubwa hapendi kuwa tegemezi ndiyo sababu ya y eye kuingia katika shughuli hiyo, inayomfanya kusimama kwa miguu yake kimaisha.
Faith anaongeza kuwa wanawake wengi wa umri wake wamekuwa tegemezi kwa watoto na wajukuu zao kuwa kutojipanga hivyo kutokuwa na shughuli za kufanya, tofauti na ilivyo kwake.
“Imekuwa ni kawaida kwa wazee wengi kuishi katika mazingira magumu kutokana na umri wao kuwazuia kufanya shughuli za kujiingizia kipato, lakini binafsi namshukuru Mungu siwezi kuwa mzigo kwa watoto wangu kwa kuwa najimudu kwa kila kitu,”anasema
Faith anasema kuwa licha ya kuwa na mume kwa wakati huo, siku zote alikuwa mtundu wa kubuni njia mbalimbali za kutafuta fedha ili kuepuka kuwa tegemezi.
“Huwa situlizi kichwa, siku zote najaribu kutafuta njia na miradi ya kuniingizia pesa ndiyo maana hata mume wangu alivyofariki sikutetereka kwa kuwa nilifahamu sitakuwa ombamba,”anabainisha.
MWANANCHI.
No comments:
Post a Comment