Friday, 21 February 2014

KISUMO AKERWA WAJUMBE "KULILIA" POSHO


 Mwanasiasa mkongwe nchini, Peter Kisumo, amesema anawasikitikia Watanzania kutokana na hatua ya baadhi ya viongozi waliowamini na kuwapa uongozi kutafunwa na kirusi cha posho.


“Kwa wanaoona posho haitoshi wajiondoe kwenye hilo bunge badala ya kuwabebesha Watanzania mzigo…. Watanzania wengi wamekerwa na mwenendo huo na inasikitisha,”alisema Kisumo.
Kisumo alitoa kauli hiyo jana kufuatia taarifa kuwa  baadhi ya wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba nao kuibuka na hoja ya  kutaka waongezewe posho wakidai kuwa kiasi cha Sh300,000 wanacholipwa kwa siku ni kidogo.
Lakini wakati wajumbe hao wakidai kuwa kiwango hicho ni kidogo, imebainika kuwa wengi wanaishi katika hoteli za kati ya Sh40,000  na Sh 80,000 kwa siku huku madereva wao wakiishi katika nyumba za kati ya Sh15,000 na 20,000.
“Inasikitisha kidogo hata kazi waliyotumwa haijaanza, baadhi yao wameanza kudai nyongeza ya posho… bahati mbaya tuna taifa ambalo baadhi ya viongozi wetu wanajali zaidi matumbo yao,”alisema Kisumo.
Kisumo aliyewahi kushika nyadhifa kadhaa katika utawala wa awamu ya kwanza, alisema kirusi hicho cha posho, kilianza katika Bunge la Jamhuri na sasa kimehamia katika Bunge Maalum la Katiba.
“Siku zote hakuna pesa inayotosha na wenzetu hawa (wajumbe) wajue kuwa hawalipwi posho hizo ili waondokane na umasikini, bungeni sio mahali pa kutajirikia ni chombo cha uwakilishi,”alisema.
Kisumo alisisitiza” bahati mbaya Bunge hili linalotakiwa kuweka historia hata halijaanza kazi limeshaanza kunukia harufu ya tamaa, wajumbe wapime kati ya uzalendo na maslahi binafsi.”
Mwanasiasa huyo alisema anamuomba Mungu amweke hai ili angalu siku moja, Watanzania waweze kuchagua viongozi walioweka mbele maslahi ya umma badala ya kutanguliza maslahi binafsi.
Hoja ya posho imeibuka wakati Watanzania wakiishi katika lindi kubwa la umasikini huku baadhi yao wakiishi kwa mlo mmoja kwa siku, hospitali zikiwa hazina dawa na shule zikiwa hazina madawati

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!