
Kesi ya madai iliyofunguliwa na aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa CHADEMA, Zitto Kabwe, dhidi ya chama hicho, itatajwa leo katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam.
Zitto alifungua kesi hiyo dhidi ya Baraza la Wadhamini la chama hicho na Katibu Mkuu, Dk. Willibrod Slaa; ambapo Zitto anaomba mahakama itoe zuio kwa kamati kuu au chombo chochote cha chama, kujadili uanachama wake hadi atakapokata rufaa ya kupinga uamuzi uliomvua uongozi wa chama.
Aidha, anaomba mahakama imwamuru Dk. Slaa ampe nakala zinazotoa sababu za uamuzi wa kumvua uongozi katika kikao kilichofanyika Novemba 22 mwaka jana, ili akate rufaa katika Baraza Kuu la Chama.
Zitto anaomba CHADEMA isiingilie kazi zake za ubunge wala uanachama wake. Kesi hiyo namba moja ya mwaka huu, itatajwa leo mbele ya Jaji John Utamwa.
Kabla kesi hiyo haijaanza kusikilizwa, mahakama hiyo imetoa amri kwa Kamati Kuu au chombo chochote cha CHADEMA kutojadili uanachama wa Zitto hadi kesi hiyo itakaposikilizwa na kutolewa uamuzi.
Katika uamuzi huo, mahakama ilikubali ombi la Zitto, ambaye ni Mbunge wa Kigoma Kaskazini, kwa kuwa hoja zake zimekidhi matakwa ya kisheria ya kutolewa kwa zuio la muda la kutojadiliwa kwa uanachama wake.
Jaji Utamwa alisema Zitto amekidhi matakwa ya kisheria, kwa kuwa zuio hilo lisipotolewa na akavuliwa uanachama, atapoteza nafasi ya ubunge na kushindwa kuwatumikia wananchi waliomchagua na pia atapoteza nafasi ya Mwenyekiti wa Bunge wa Kamati ya Kudumu ya Hesabu za Serikali.
Zitto alivuliwa wadhifa wake CHADEMA, sambamba na aliyekuwa mjumbe wa Kamati Kuu, Dk Kitilla Mkumbo na Mwenyekiti wa Mkoa wa Arusha, Samson Mwigamba, kwa kilichodaiwa ni usaliti kwa chama hicho cha upinzani.
DAR 24...













No comments:
Post a Comment