Saturday, 15 February 2014

ARV ZAUZWA MITAANI MKOANI MARA.

Dawa za Kurefusha Maisha ya Waathirika wa Ukimwi ARV
 Imebainika kuwa dawa za Serikali zikiwamo za kurefusha maisha kwa waathirika wa Ukimwi zinauzwa katika maduka ya dawa baridi na maduka bubu ya watu binafsi katika Wilaya ya Rorya mkoani Mara. Uchunguzi wa gazeti hili umebaini kuwa maduka yanayouza dawa hizo mengi yanamilikiwa na watumishi katika vituo vya afya vya Serikali, wakati dawa zinazouzwa ni zile ambazo hutolewa na Serikali kwa ajili ya kupelekwa kwenye Zahanati na Vituo vya Afya kwa ajili ya wagonjwa.
Uchunguzi zaidi umebaini kuwa afya za wanunuzi na watumiaji wa dawa katika maduka husika ziko hatarini kutokana na mazingira yasiyoridhisha ya maduka husika, huku wahudumu au wauzaji katika maduka hayo wakibainika kuwa kuwa si watu wenye elimu ya ufamasia.

Katika Kijiji cha Changuge kata ya Mirare, ilibainika kuwa dawa zikiwamo ARV zinapatikana kwa urahisi katika duka linalomilikiwa na mtumishi anayefahamika kwa jina la Nicolaus Joseph, ambaye ni Muuguzi wa Kituo cha Afya cha Serikali, Changuge.
Uchunguzi huo pia ulibaini kwamba dawa hizo pia zinauzwa katika duka la mtumishi mwingine wa kituo hicho, Pamela Otuma ambalo liko katika Kijiji cha Nyambogo, Kata ya Kitembe Wilayani Rorya.
Hata hivyo, Joseph na Otuma kwa nyakati tofauti walikanusha kuuza dawa za ARV pamoja na nyingine, licha ya kila mmoja wao kukiri kwamba aliwahi kumiliki duka la dawa siku zilizopita.
Joseph alisema duka la dawa alilikuwa akilimiliki lilifungwa Februari mwaka jana baada ya kubainika kwamba kufunguliwa kwake hakukufuata taratibu za kifamasia.
“Nilikuwa na duka ambalo lilikuwa likiniingizia kipato cha ziada, lakini sikuwahi kuuza dawa za Serikali, hata hizo tuhuma zilipotolewa ukaguzi ulifanyika na sikukutwa na dawa zozote kwenye duka,” alisema Joseph na kuongeza:
“Baada ya kufungiwa niliuzwa dawa zilizokuwepo kwa watu wengine wenye maduka na hivi sasa najiandaa kufuata taratibu za kifamasia ili niweze kufungua tena duka langu”. Kwa upande wake Otuma alisema : “Mimi sijawahi kuuza dawa za Serikali katika duka langu, na duka hilo lilikuwa Kijiji cha Nyambogo lakini kulipoanza kuwepo maneno kwamba nauza dawa za Serikali nikalifunga”.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Rorya, Ephraem Ole Nguyaine alisema malalamiko ya kuuzwa kwa dawa hizo nje ya taratibu yamefika ofisini kwake na kwamba ilikuwa sababu ya kuhamishwa kwa watumishi wa afya akiwamo aliyekuwa Mganga Mkuu wa wa Wilaya hiyo, Daniel Chacha.
“Ninashangaa dawa hizo kudaiwa kuwa bado zinaendelea kuuzwa katika maduka ya mitaani, kwa kweli nitafuatilia zaidi suala hili,” alisema Ole Nguyaine.
Wanaoshi na VVU
Baadhi ya watu wanaoishi na Virusi vya Ukimwi walikiri kununua ARV na dawa nyingine katika maduka hayo ya watu binafsi kutokana na kile walichokieleza kuwa ni uhaba wa dawa hizo katika vituo vya Serikali.
MWANANCHI

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!