Saturday, 18 January 2014

SERIKALI IMEKUSANYA SH BILION 377.4 KUTOKANA NA MAUZO YA GESI.



SERIKALI imekusanya Sh bilioni 377. 4 kutokana na mauzo ya gesi asilia nchini katika kipindi cha kuanzia Julai 2004 hadi Oktoba mwaka jana.



Akizungumza na gazeti la Habari Leo Dar es Salaam hivi karibuni, Mkurugenzi wa Masoko na Uwekezaji katika Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Injinia Joyce Kisamo alisema fedha hizo ni jumla ya mauzo ya gesi asilia kwa taasisi, watu binafsi na viwandani.
Miongoni mwa wateja wakuu aliowataja ni pamoja na Shirika la Umeme la Taifa (TANESCO), Hoteli ya Serena iliyoko Dar es Salaam na nyumba zaidi ya 50 zilizounganishiwa gesi hiyo kupitia mradi wa majaribio kwenye eneo la karibu na viwandani, Mikocheni Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa Kisamo, mapato hayo yanategemewa kuongezeka zaidi katika miaka ijayo kutokana na kupanuka kwa soko la gesi asilia nchini pamoja na kuongezeka kwa matumizi ya nishati hiyo kila siku.
Aidha Kaimu Mkurugenzi wa Utafiti, Uendelezaji na Huduma za Kitaalamu wa TPDC, Ema Msaky alisema pato litaongezeka kwa sababu upo uwezekano mkubwa wa kuongezeka kwa gesi kutokana na dalili mbalimbali zinazoonekana katika utafiti.
Hata hivyo, pamoja na kuwepo kwa mafanikio hayo, imeelezwa kuwa nchi inapata hasara ya Sh trilioni 1.6 kwa mwaka kutokana na kutumia mitambo ya dharura ya uzalishaji umeme inayotumia mafuta badala ya gesi asilia.
Kamishna wa Nishati na Masuala ya Petroli, Hosea Mbise alimwambia mwandishi wa habari hizi, hali hiyo ndiyo iliyosababisha Serikali kujenga bomba la kusafirisha gesi asilia kutoka Mtwara, Songo Songo hadi Dar es Salaam, ili kuweza kupata gesi ya kutosha kwenye mitambo yake kwa lengo la kuokoa fedha zake.

HABARI LEO

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!