
WAZIRI Mkuu, Mizengo Pinda, ametembelea makazi na ofisi zilizochomwa moto wakati wa vurugu za gesi mkoani Mtwara na kuelezewa baadhi ya sababu za vurugu hizo. Akielezea sababu hizo, Mkuu wa Wilaya Masasi, Farida Mgomi alisema moja ya sababu za vurugu katika Mji wa Masasi na vitongoji vyake, ni madai na uchochezi kwamba viongozi wa CCM katika wilaya, wameshindwa kuwajibika kwa wananchi.
Mgomi alisema wananchi waliona kwamba viongozi wameshindwa kuisimamia Serikali; wakakosa imani na uongozi wa chama hali iliyosababisha kuingia mitaani na kuchoma moto nyumba za viongozi wakiwemo wabunge.
Mkuu huyo wa Wilaya alimweleza Pinda mara alipofika nyumbani kwa Mbunge wa Viti Maalum na aliyekuwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wanawake ya CCM (UWT) Taifa, Anna Abdallah ambaye nyumba yake pia ilichomwa moto siku ya vurugu.
Vurugu hizo pia zilisababisha kuchomwa kwa nyumba ya Mbunge wa Masasi Mariamu Kasembe na ofisi ya CCM ya Wilaya na kuchoma magari ya Halmashauri ya Wilaya ya Masasi na ya watumishi wake na Mahakama ya Mwanzo Masasi.
Pia katika vurugu hizo kituo kidogo cha Polisi, kilichomwa moto. Katibu wa CCM Mkoa wa Mtwara, Shaibu Akwilombe alipoulizwa juu ya taarifa hiyo ya DC wa Masasi alisema “hayo ni maoni ya Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya.”
Lakini Akwilombe alishangazwa na taarifa hiyo ya DC kwa kushindwa kukiri kuwa kulikuwa na tatizo kubwa kati ya Polisi wa Usalama Barabarani na waendesha bodaboda ambao alidai ndicho kilikuwa chanzo cha vurugu hizo.
“Sisi hatupingi maoni yao, lakini nashangaa tu kwamba kwa nini ameshindwa kuliweka hilo la Polisi na waendesha bodaboda,” alisema Akwilombe alipotakiwa na gazeti hili kutoa maoni yake.
Alipohojiwa na waandishi wa habari kuhusu madai ya kuwepo mvutano kati ya polisi na waendesha pikipiki, Mgomi alisema ugomvi huo sio mkubwa wa kusababisha vurugu zile bali vyanzo ni hivyo alivyovitaja kwa Waziri Mkuu.
Mgomi alitaja sababu nyingine ni kutokana na wananchi kucheleweshewa malipo ya korosho mara wanapouza mazao yao kwa vyama vya ushirika, na uchochezi uliofanywa na baadhi ya wanasiasa kuhusu masuala ya gesi.
Wanasiasa hao wanadaiwa kuwachochea wananchi kuwa hawatafaidika na gesi hiyo badala yake inachukuliwa na Serikali na kwenda kuwanufaisha watu wa Dar es Salaam na Bagamoyo.
Alitaja sababu nyingine iliyosababisha vurugu hizo ni ugumu wa maisha unaowakabili wananchi hivyo wanasiasa kutumia fursa hiyo kupenyeza ajenda zao za siri na kuamsha hasira ya wananchi dhidi ya Serikali na chama tawala.
Pinda akizungumza mbele ya ofisi ya CCM iliyoungua katika vurugu hizo alikiri kuwa kuna watu walitumia fursa ya Serikali kuchelewa kutoa elimu kwa wananchi juu ya suala la gesi, hivyo wakawachochea wananchi juu ya suala hilo.
“Kuna watu walipotosha kwamba ile gesi inaenda Bagamoyo kwa Rais Jakaya Kikwete jambo ambalo lililazimu mimi kuja hapa nikafanya kikao na wadau mbalimbali hadi tukapata suluhisho la suala hili,” alisema Pinda.













No comments:
Post a Comment