Thursday 23 January 2014

MAFURIKO YAIKUMBA DUMILA KILOSA MAMIA WAATHIRIKA NA DARAJA KUVUNJIKA

Wananchi wa Dumila mkoani Morogoro wakitumia uzoefu wao wa kuogelea kujinusuru na mafuriko yaliyotokea jana na kuhatarisha maisha ya watu wengi ikiwa ni pamoja na kuharibu madaraja.
Mafuriko makubwa yametokea katika Kata ya Dumila, Kilosa mkoani Morogoro na kusababisha mamia ya watu kupoteza makazi huku daraja la Mto Mkundi linaloziunganisha Wilaya za Kilosa na Mvomero likivunjika.
Mafuriko hayo yalisababishwa na mvua kubwa zilizoanza kunyesha jana alfajiri na kusababisha maafa makubwa yakiwamo kuharibiwa kwa makazi ya watu, majengo ya Serikali zikiwamo shule, vyuo na mahakama.
Habari zinasema mafuriko hayo pia yalichangiwa na mvua kubwa iliyoanza kunyesha usiku wa kuamkia jana katika sehemu za milima iliyopo Kilosa na Mvomero, hivyo Mto Mkundi kushindwa kuhimili maji hayo.
Mashuhuda walisema waliona maiti ya mtu ikielea kwenye maji yaliyokuwa yakipita kwa kasi, tukio ambalo lilithibitishwa na Diwani wa Kata ya Magole, Juma Rajabu Chewe. Chewe alisema maiti hiyo ilionekana ikielea eneo la Mateteni na kwamba taarifa zilitolewa polisi ili aopolewe. Hadi jana jioni idadi ya watu walioathiriwa na maafa ilikuwa bado haijafahamika.
Maji yasambaa kwenye vijiji mbalimbali vinavyozunguka mto huo na kuwalazimisha baadhi ya watu kulazimika kujiokoa kwa kupanda kwenye paa za nyumba zao huku wengine wakikwea juu ya miti.
Baadhi ya watu walikutwa na mafuriko hayo mashambani na walipozidiwa na nguvu ya maji walijiokoa kwa kushikilia vitu mbalimbali ikiwamo miti, huku baadhi yao wakipoteza nguo walizokuwa wamevaa walipokuwa kwenye harakati za kujiokoa.
Polisi waliofika eneo hilo kwa ajili ya uokoaji walilazimika kuomba helikopta kutoka makao makuu ya jeshi hilo, Dar es Salaam ili kuwaokoa watu waliokuwa kwenye paa za nyumba na kwenye miti iliyokuwa imezungukwa na maji.
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Joel Bendera alitaka kuwapo kwa uvumilivu wakati Serikali ikiendelea na taratibu za kuwaokoa walioko juu ya miti na kutoa misaada kwa walioathirika.
Alisema kuwa kutokana na hali kuwa mbaya, ofisi yake ililazimika kuomba helikopta kwa ajili ya kuongeza nguvu ya juhudi za uokoaji.
Taharuki kubwa
Mafuriko hayo yalizua taharuki kubwa kiasi cha wananchi kutawanyika ovyo wakiwa hawajui cha kufanya, kutokana na nyumba zao kuharibiwa na mali zao hususan mazao yakisombwa na maji.
Hali ilikuwa mbaya zaidi kwa kina mama wakiwa na watoto ambao walionekana katika makundi wakiomba msaada baada ya kukimbia makazi yao, huku wengi wakiwa wamelowa kutokana na kunyeshewa
MWANANCHI.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!