WAZIRI wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk Shukuru Kawambwa, ametaka wanaobeza kazi ya wizara yake kujitokeza kupongeza kwa ufaulu wa mitihani ya wanafunzi wa darasa la saba.
Dk Kawambwa alisema hayo katika hotuba yake ya kufungua kikao cha kazi cha maofisa elimu wa mikoa ya Tanzania bara na wa halmashauri za wilaya jana mjini Morogoro.
Kutokana na mafanikio hayo katika sekta ya elimu hasa ya kuongeza kiwango cha ufauli wa wanafunzi, Waziri Kawambwa alibeza wapinga maendeleo na kuwataka kutambua suala hilo kwa kutoa pongezi kwa kazi kubwa inayofanywa na watendaji wa Wizara kuinua kiwango cha elimu nchini.
“Wanaotusema vibaya na kutishia kuandamana barabarani wakitaka Waziri mwenye dhamana ajiuzulu pale wanapoona kasoro, sasa wafanye hivyo kwa kutupongeza katika hili la kuongeza kiwango cha ufaulu kutoka asilimia 31 mwaka jana hadi 50.61 mwaka huu, wako kimya...ongezeko la asilimia 20 haliokenani!” alishangaa Waziri Kawambwa.
Hata hivyo, alisema licha ya kutofikiwa lengo ya BRN la asilimia 60 kwa mwaka 2013, juhudi zinaendelea kufanywa zaidi katika usimamizi na uwajibikaji, ili kufikia malengo yaliyowekwa kwa miaka ijayo na kuwa uwezekano ni mkubwa wa kufikia asilimia 80 ya ufaulu ifikapo mwaka 2015.
Pamoja na hayo, alisema mafanikio hayo makubwa sasa yanapaswa kupongezwa na Watanzania wote, licha ya sasa kubatizwa jina la ‘Waziri Mzigo’, jambo ambalo hawezi kulikwepa kama kiongozi mkuu wa wizara hiyo.
Kwa mujibu wa Waziri huyo, utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Msingi (MMEM) na ule wa Elimu ya Sekondari (MMES) imeonesha pia mafanikio makubwa.
“MMEM imeonesha mafanikio katika uandikishaji wanafunzi shule za msingi, ambapo hadi mwaka 2012, idadi yao ilikuwa 8,247,172 huku idadi ya shule za msingi ikiwa 16,331,” alisema Dk Kawambwa.
Kwa upande wa MMES, idadi ya wanafunzi imeongezeka kutoka 524,325 mwaka 2005 hadi 1,884,272 mwaka 2012 na kupitia BRN uboreshaji wa mazingira ya kufundishia na kujifunzia ni mojawapo ya mikakati ya kipaumbele.
Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Profesa Sifuni Mchome, alisema vijana milioni 11 wapo shuleni na elimu inayotolewa inahitajika iwe bora zaidi itakayoleta mabadiliko kwa watoto kielimu.
Kwa mujibu wa Katibu Mkuu huyo, asilimia tatu ndio wanapata elimu ya kiwango cha ubora wa juu zaidi, wakati asilimia 10 wanapata elimu yenye ubora wa kati na asilimia 87 hawapati elimu bora na kutaka kuanzia sasa ubora wa elimu uzingatiwe kwa kuwa na vitendea kazi stahiki.














No comments:
Post a Comment