Thursday 26 December 2013

TANGA WATAHADHARISHWA KUHUSU KUWEPO KWA KIMBUNGA

DSCN7186Wakazi wa Jiji la Tanga wametahadharishwa kuwepo kwa mchafuko wa bahari, hali inayotokana na kuimarika kwa mgandamizo mdogo wa hewa katika Bahari ya Hindi na Visiwa vya Comoro.


Kufuatia hatua hiyo, wananchi wote hususan wavuvi na waogeleaji baharini wanaagizwa kuchukua ahadhari kubwa ili kuepusha madhara yanayoweza kujitokeza.
 
Akizungumza katika mahojiano na NIPASHE, Mkuu wa Wilaya ya Tanga, Halima Dendego, alisema kuwa kwa mujibu wa taarifa walizozipata kutoka Mamlaka ya Hali ya Hewa  Tanzania (TMA), hali hiyo itapelekea bahari kuwa na mawimbi makubwa sambamba na upepo mkali.
 
Dendego alisema kuwa mabadiliko hayo ya hali ya hewa yanataraji  kuukumba Mji wa Tanga kuanza juzi jioni hadi Desemba 26 leo, hivyo wananchi wachukue tahadhari kwenye maeneo ya Pwani.
 
“Tunajua kuwa starehe yetu watu wa Tanga ni kutembea katika fukwe na wengine kuogelea. Vilevile, shughuli za kiuchumi ikiwemo uvuvi hufanyika baharini hivyo natoa wito kwa wananchi kuchukuwa tahadhari na kama inawezekana kutofika kabisa kwenye maeneo hayo,” alisema.
 
Nao baadhi ya wavuvi wakizungumza katika mahojiano na NIPASHE, walisema kuwa mpaka sasa wapo baadhi ya wenzao ambao walienda baharini na hawajarudi na hawana uhakika wa usalama wao kwani kumekuwa na mchafuko mkubwa wa bahari.
 
“Ni kweli kumekuwa na mchafuko mkubwa sana wa bahari si unaliona wimbi hilo linavyovuma na kuna wenzetu walienda baharini jana (juzi) hatujui hatma yao,” alisema Mbaruku Jumaa.
 
Hata hivyo, walisema kuwa wameshatoa taarifa kwenye mamlaka husika na kwamba hatua za ufuatiliaji zimeanza kuchukuliwa ili kubaini iwapo kuna waliopata madhara kutokana na machafuko hayo.
CHANZO: NIPASHE

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!