Tuesday, 31 December 2013

KUTANA NA VIJANA WALIOJIAJIRI WENYEWE JIJINI DAR, USINGOJE KUAJIRIWA PENYE NIA PANA NJIA.....

NA HAWA NDIO VIJANA WANAOJIAJIRI WENYEWE YAANI WAJASIRIAMALI LIVE!!


Tangu waiingize teknolojia hiyo mpya nchini, wamepokea kazi nyingi za kufanya usafi kwenye majengo mengi nchini hasa katika Jiji la Dar es Salaam. 

  • Lengo kuu la kuanzisha Shirika la TZAID ni kwamba liwe kama lilivyo Shirika la USAID, yaani liwe ni Shirika la Watu wa Tanzania.Wakati utafika TZAID itakuwa inakwenda nje ya nchi kutoa misaada ya aina mbalimbali ikiwemo kuwatuma wasomi wa Tanzania kuendesha mafunzo yakiwemo ya ujasiriamali na kadhalika, kisha watakuwa wanajulikana kama Watu wa Tanzania

Watu wengi wanapenda kuwa na maisha bora, wengi wanaishia kuwa na hali duni. Baadhi ya watu wamekuwa wakijiuliza ‘kwa nini ninakuwa na maisha duni’, ingawa jibu lake ni kwamba adui wa kwanza wa maisha yako ni wewe mwenyewe…Kukata tamaa kwako.
Je, wewe unayesoma makala haya una hali gani ya maisha? Kila mtu analo jibu lake. Kwa vyovyote unavyoweza kujibu, kitu ambacho unapaswa kubaki nacho katika akili yako ni kwamba hatima ya maisha yako itatokana na matendo yako; huwezi kupanda bangi shambani mwako halafu unakatarajia kuvuna mpunga; utavuna kile ambacho unakipanda.
Tunapoelekea kuumaliza mwaka 2013 na kuingia mwaka 2014 ni suala la msingi sana kutafakari namna unavyoishi, ni lazima mwanadamu awe tofauti na mnyama, apate muda wa kujitathmini namna anavyoishi na kuona kama yuko sahihi au la, wapi ajirekebishe ili mambo yaweze kwenye mbele.
“Kati ya mambo ambayo nawaasa sana vijana na Watanzania kwa ujumla kujitazama nayo ni kuhusiana na suala zima la kipato, maisha ya wengi yanakuwa duni kwa sababu ya wao wenyewe kushindwa kuthubutu kufanya mambo. Wengine ni wepesi wa kukata tamaa,” anasema Khamis Tembo, mmoja wa viongozi katika taasisi yenye kutoa huduma mbalimbali zikiwemo za kufanya usafi.
Tembo anasema yeye na vijana wenzake waliohitimu vyuo mbalimbali nchini wamelazimika kuanzisha taasisi waliyoipa jina la TZAID; Tanzania Agency for International Development, yaani Shirika la Msaada la Watu wa Tanzania kama lilivyo lile la Watu wa Marekani (USAID), azma ni kuisaidia jamii, pia kuitangaza Tanzania nje.
“Ni kutokana na tatizo la ajira tuliona tuungane vijana kutoka katika vyuo mbalimbali, ndipo mwaka jana tukaamua kuanzisha shirika hili ambalo kwa kweli limepokelewa vizuri na watu mbalimbali nchini,” anasema Tembo ambaye ni Mkurugenzi wa Miradi katika shirika hilo.
Anasema mojawapo ya huduma ambazo zinaendeshwa ni kutoa elimu ya ujasiriamali na utengenezaji wa bidhaa mbalimbali zikiweko vyakula vya mifugo ikiwemo kuku na namna ya kuendesha ufugaji bora.
“Tunaendesha pia mafunzo kwa njia ya semina na ana kwa ana juu ya namna ya kuanzisha na kuendeleza miradi mbalimbali kwa mafanikio. Tumepokea barua kutoka kwa wabunge na viongozi kadhaa ambao wamekuwa wakitushawishi twende kwenye maeneo yao kuendesha mafunzo ya utengenezaji wa bidhaa zikiwemo sabuni, mishumaa, shampoo, mikate, batiki  na nyingine nyingi. Tulikuwa kwenye hatua nzuri za kwenda Sudani ya Kusini kwa ajili ya kuendesha mafunzo ya namna ya kutengeneza bidhaa mbalimbali kwa nchi nzima, kwa bahati mbaya hali ya usalama kwa sasa si nzuri, hata hivyo tunajipanga kuangalia  namna gani tunaweza kwenda kuendesha mafunzo hayo,” anasema Tembo.
Mwanzoni mwa mwaka huu waliamua kuanzisha mradi wa kufanya usafi hasa baada ya kupata teknolojia ya kufanya usafi kutoka Malaysia. “Tulipata msaada wa elimu ya usafi kutoka Kampuni ya Mosa inayojihusisha na teknolojia iitwayo Mosa ya usafi wa aina mbalimbali hasa ule uchafu mgumu ulioshindikana,” anafafanua Tembo.
Tangu waiingize teknolojia hiyo mpya nchini, wamepokea kazi nyingi za kufanya usafi kwenye majengo mengi nchini hasa katika Jiji la Dar es Salaam.
“Tumepokea tenda nyingi na tunashukuru kwamba kwa sababu tunao wafanyakazi wengi, haitupi shida kufanya kazi hizo, kwa sasa tunajipanga kuelekea Tanga kwa ajili ya kufanya mazungumzo na baadhi ya viongozi wa Serikali ili kuangalia namna gani tunaweza kuwasaidia katika harakati zao za kuwasaidia watu kuwa na maisha bora, kupitia kuendesha wa ujasiriamali na utengenezaji bidhaa mbalimbali,” anafafanua.
Aidha Ofisa Uhusiano wa TZAID, Robert Kidogi anasema mkakati uliopo kwa sasa ni kuzisambaza huduma zao ndani na nje ya Dar es Salaam, pamoja na nchi jirani, kwani teknolojia hasa za usafi walizonazo ni ngeni.
“Kuna watu nyumba zao ni chafu mno au unaweza kuona hata injini ya gari labda ni chafu mno au mtambo fulani, sisi kupitia hii teknolojia tunaweza kusafisha na uchafu hata kama ni mgumu kiasi gani ukatoka,” anafafanua Kigodi.
MAISHA BORA YANAWEZEKANA
Kigodi anawaasa vijana nchini kutokukata tamaa hasa pale wanapokuwa na hali ngumu au kukosa ajira, badala yake siku zote wawe wanatafakari ili kuangalia namna gani watakuwa na mafanikio.
“Mimi nimefanya kazi katika maeneo kadhaa, lakini ukweli sikupendezwa na hali ya malipo, najua ni wengi ambao wanafanya kazi kwa malipo madogo wanavumilia, kitu ambacho siyo sahihi, ni lazima siku zote tuangalie na kuwa wabunifu, hakika tutafanikiwa,” anasema.
Anafafanua kwa mfano mtu unakuta labda amesoma hadi shahada ya kwanza au hata ya pili, anacholipwa kwa  siku haizidi Sh10,000 kiasi ambacho ni kidogo ukilinganisha na hali ngumu ya maisha iliyoko nchini.
“Sisemi waache ajira, ila ninachosisitiza ni kwamba ni vizuri wakawa wabunifu, mfano mtu akiamua kufuga kuku wa kisasa, akawa na kuku wake 3000 tu akiwauza  labda kwa Sh7000  ni kwamba anaweza kupata Sh21 milioni…hata akitoa matumizi siyo rahisi kukosa Sh10 milioni,” anafafanua na kuwataka vijana na Watanzania kwa jumla kuyatafakari sana maisha.
Kidogo anasema lengo la shirika ni kutoa elimu ili hatimaye watu waweze kujitambua na kutambua miradi mizuri ya kufanya, ikiwemo kuchukua nje teknolojia ambazo nchini hazipo ili ziweze kusaidia kuharakisha maendeleo.
“Kwa mfano teknolojia tuliyonayo ya kusafisha majengo na mitambo, ni ngeni, ndiyo kwanza tumeiingiza kupitia hao washirika wetu wa Mosa, wengi wanaitumia na wanaifurahia,” anasema Kigodi na kufafanua kuwa kuna vijana wengi na Watanzania wengine wengi ambao wamekuwa wakienda nje, wanaona teknolojia mbalimbali hawaoni umuhimu wa kuzileta nchini, kitu ambacho siyo sahihi.
MRADI MAALUM WA KUINUA WATU KIUCHUMI
Kidogi anasema wamekuwa wakitoa ushauri na elimu kwa mtu mmoja au kikundi  kuhusu namna ya kuanzisha shughuli zake za maendeleo, pia kuendesha elimu ya utengenezaji wa bidhaa.
Elimu wanayotoa imekuwa na maana kubwa kwa sababu ya ukweli kwamba imesababisha vijana wengi na watu wazima kuanzisha miradi ya maendeleo.
“Kwa mfano kutengeneza keki ni rahisi mno, unachanganya unga wa ngano, sukari, mayai na kadhalika, kwa uwiano maalumu kulingana na vile ambavyo mtu anapenda, au kutengeneza batiki na bidhaa zingine.
“Hakuna sababu kijana au mtu yeyote kushindwa kuanzisha mradi wa aina yoyote.
“Unakuta wengine wake zao hawafanyi kazi zozote, hili ni kosa kubwa, kwani hii ni ishara kwamba mume akifa, hiyo nyumba itakuwa na maisha duni mno.Tunashukuru kwamba viongozi mbalimbali wakiwemo baadhi ya wabunge, wakuu wa wilaya na  kadhalika nchini wamekuwa wakituomba kuendesha elimu katika maeneo yao. Mfano tunatarajia wiki ijayo kwenda kuonana na kiongozi mmoja wa Kiserikali Tanga ili kuangalia namna gani anatutumia kuendesha mafunzo yetu kwa watu wake,” anafafanua Kidogi.  Baadhi ya wananchi waliopewa huduma za shirika hilo wanasema kwamba likisaidiwa linaweza kuwa mkombozi mkubwa wa wananchi wa Tanzania.
“Mimi nimepata huduma za shirika hili la TZAID, ukweli ni kwamba nimebadilika tayari kimaisha, kwa maana kwamba sasa nafuga kuku wengi tu maeneo ya Pangani, Kibaha, maisha yangu yamebadilika hadi nimelazimika kuachana na kazi ya uuguzi niliyokuwa nikifanya kwa miaka mingi,” anasema Hamisa Khalfan katika mahojiano na mwandishi wa makala haya.
Hamisa anawashauri watu kuwa na mwamko wa kuwasaidia watu walioko kwenye maeneo yao; mfano unaweza kutoa msaada wa kuendeshwa kwa elimu kwa watu wa eneo ulilozaliwa au watu ambao ungependa wabadilike kimaisha.
“Nilikozaliwa ni  Tanga, baada ya kuona nimefanikiwa nimewaalika hawa vijana wa TZAID waende kuendesha elimu ya ujasirimali na utengenezaji bidhaa katika maeneo yangu, hii ni sadaka yangu kwa watu wangu,” anasema.
Aidha Mkurugenzi wa Miradi katika shirika hilo la TZAID, Khamis Tembo anawasisitiza kuwa “Kila mtu akiwa chanzo cha mabadiliko anayotaka kuyaona Tanzania, maendeleo yatakua kwa haraka.

LEMUTUZ

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!