skip to main |
skip to sidebar
WACHINA NA PEMBE ZA NDOVU: MAMLAKA ZETU ZINAFANYA KAZI IPASAVYO?
Wiki hii raia watatu wa China walikamatwa kwenye nyumba moja katika eneo la Mikocheni mjini Dar es Salaam, wakiwa na vipande 706 vya pembe za ndovu. Tukio hili limetokea siku chache baada ya mchina mwingine kukamatwa katika uwanja wa ndege akijaribu kusafirisha vipande 41 vya pembe za ndovu.
Kukamatwa kwa watu hao kumeibua tena mjadala kuhusu tatizo la ujangili linalozikabili nchi za Afrika Mashariki, hasa kwa wakati huu ambapo serikali ya Tanzania imetangaza kuwa italivalia njuga tatizo la ujangili na biashara ya pembe za ndovu. Kila mara tukio la usafirishaji wa pembe za ndovu linapotajwa maneno Asia, husuan China na Wachina pia yanatajwa.

Kwa watu wanaofuatilia tatizo la ujangili na biashara ya pembe za ndovu, iwe ni Tanzania au katika eneo zima la Afrika Mashariki, tukio hili si jambo jipya na si kubwa kuliko yaliyowahi kutokea huko nyuma. Mwezi Oktoba mwaka jana mamlaka za Hong Kong zilikamata vipande 1,209 vya pembe za ndovu kwenye bandari ya mji huo ndani ya kontena lililotoka bandari ya Dar es Salaam. Mwezi Julai mwaka 2006 vipande 350 vya pembe za ndovu vilikamatwa kisiwani Taiwan vikiwa njiani kutoka Tanzania kwenda mjini Manila, nchini Philippines. Nchini Tanzania na Kenya kumekuwa na matukio ya mara kwa mara ya kukamatwa kwa watu kutoka nchi za Asia wakijaribu kusafirisha pembe za ndovu.
Muhimu zaidi ni kama msemo wa Kiingereza unavyosema “it takes two to tango”, watanzania tunatakiwa kuwa wakweli kama tunataka kupambana na ujangili. Tukiangalia kwa undani tukio hili, tutajiuliza maswali haya: je, inakuwaje mchina ana uwezo wa kusafirisha pembe za ndovu kutoka Manyara, Morogoro na Rukwa na kufika Dar es salaam bila kusaidiwa? Inakuwaje meli ipakie makontena ya pembe za ndovu kwenye bandari yetu bila idara husika kujua? Tukiangalia suala hili kwa mtindo wa kusema “aliyeshikwa na ngozi ndiye aliyekula nyama”, basi tutatakuwa hatujitendei haki na matukio kama haya yataendelea kutokea. Wakati tunatafakari hili, si vibaya kama tukiiuliza serikali yetu ilifanya nini kushughulikia matukio yaliyopita, nani alikamatwa na nani alichukiliwa hatua gani. Kama hakuna majibu ya maana, basi huenda tutakuwa tunamwadhibu aliyeshikwa na ngozi na anayekula nyama ataendelea kupeta.
China imekuwa soko kubwa la pembe za ndovu kuanzia mwaka 2009, kabla ya hapo soko kubwa lilikuwa Japan na nchi nyingine za Asia kusini mashariki ambazo pia zina wateja haramu wa pembe za ndovu, na hata wanaosafirisha pembe hizo kutoka Tanzania na nchi nyingine za Afrika mashariki. (kama raia wa Vietnam aliyekamatwa Agosti 16 katika uwanja wa ndege Dar es Salaam).
Labda kwa vile baadhi ya watu wanavyofikiria, China ingekuwa ni nchi ambayo pembe za ndovu zinauzwa kila mahali, na kila mtu anaishabikia bidhaa hiyo, lakini ajabu ni kuwa, kwa vile ninavyoona hapa China picha ni tofauti kabisa na jinsi baadhi ya watu wanavyodhani.
Nimesoma ripoti moja miezi kadhaa kabla ya kutokea kwa matukio ya kukamatwa kwa Wachina. Ripoti hiyo iliyotolewa na shirika la WildAid inaonesha asilimia 98.2 ya wakazi wa Beijing wanaiunga mkono serikali kuweka sheria inayozuia kabisa biashara ya bidhaa za pembe za ndovu, ikiwemo biashara ya ndani, na asilimia 99.2 ya watu waliohojiwa wanakubali tunatakiwa kuhakikisha tembo waendelea kuishi kwenye sayari yetu. Takwimu hizi ni tofauti sana na watu wengi wanavyotegemea. Je, nchi ambayo inajulikana kama soko kubwa zaidi la pembe za ndovu, inakuwaje wananchi wake wanapinga biashara hiyo?
Yeyote akikaa nchini China kwa siku kadhaa atajua sababu. Nchini China mfano mjini Beijing, pembe za ndovu na bidhaa zinazotengenezwa nazo ni nadra sana, unaweza kuziona tu kwenye duka moja kubwa katika mtaa wa biashara unaojulikana kama Wang Fu Jing,ambapo bei zake ni kubwa, mfano kinyago kilichotengenezwa meno nzima kinauzwa kwa Yuan milioni 1.7, sawa na dola elfu 280 za kimarekani, kwa hiyo bidhaa za aina hiyo si za kawaida nchini China, na ziko mbali na wachina wa kawaida. Anayedhani huu mchezo wa matajiri, basi anakosea pia. Sisi watanzania wengi wanadhani kuwa biashara ya pembe za ndovu nchini China, ni biashara iliyopewa baraka na serikali ya China. Ukweli ni kwamba kuanzia mwaka 1989 mkataba wa kimataifa ulipiga marufuku biashara ya pembe za ndovu, ambapo China ni miongoni mwa nchi 175 duniani zilizosaini mkataba huo.
Serikali ya China inapinga vikali ujangili na biashara ya pembe za ndovu. Hata baada ya habari ya wachina kukamatwa ilipofika hapa China, Wizara ya mambo ya nje ya China ililaani vikali tukio hilo. Pamoja na kuwa kwa sasa China ni soko kubwa zaidi la pembe za ndovu, lakini ununuaji wa pembe za ndovu hapa China unafanyika kwa njia haramu. Sheria za China zinatoa adhabu kali kwa watu wanaofanya kinyume cha sheria biashara ya pembe za ndovu, kiasi kwamba wahalifu wanaweza kupewa kifungo cha maisha.
Habari kuhusu wachina kukamatwa na pembe za ndovu mjini Dar es salaam, ilienea kwa kasi na wachina wengi wamelaani vikali na kuonesha kukasirishwa na kitendo hicho.
Yeyote akijua Kichina anaweza kufungua tovuti ya Microblog ya China inayojulikana kama WEIBO, ambayo inafanana na Twitter na kutumiwa na wachina zaidi ya milioni 500, na kutaipu HIFADHI TEMBO(bila shaka kwa kichina) utaziona post hii imetolewa maoni zaidi ya mara elfu 75, na ukitaipu SEMA HAPANA KWA BIASHARA YA PEMBE ZA NDOVU, utaona post hii imeitikiwa zaidi ya mara elfu 570, wengine wanasema sijawahi kununu bidhaa za pembe za ndovu, na hakuna aliye karibu nami aliwahi kununua bidhaa hiyo, je, bishara inanihusu vipi? Wengine wanapinga wakisema hata kama hatununui bidhaa za aina hiyo, lakini bado tunahusika wote na kazi ya hifadhi ya wanyama. Wengine wanasema Bila Biashara, Hakuna Mauaji, mwito ambao ulitolewa na mchezaji wa mpira wa kikapu wa China Yao Ming, na kujulikana karibu kila mtu nchini China.
Nilipomwuliza rafiki yangu mmoja aliyewahi kukaa nchini Tanzania kwa miaka mitatu aliniambia alikuwa na fursa nyingi za kununua pembe za ndovu na bidhaa zinazotokana nazo, kwa kuwa “ukiwa mchina, biashara itakujia mwenyewe na kugonga mlango wako”. Lakini msichana huyo wenye umri wa miaka 28 aliniambia hakununua hata moja, kwa sababu anataka kuwaambia wafanyabiashara hao, ambao mara nyingi ni wenyeji, kwamba si kila mchina anashabikia bidhaa hiyo inayosababisha maumivu na mauaji. Tukiwa watanzania tungeona haya. Wakati tunapowalaumu wachina kwa biashara haramu za pembe za ndovu na kuilaumu serikali yetu kwa kuangalia mikono kifuani, tunatakiwa kujiuliza, je, ni wachina wanaoua ndovu wetu au ni wazo letu la kwamba wachina wanapenda kununua pembe za ndovu linaloua ndovu wetu?
- .fikrapevu.com/
No comments:
Post a Comment