Sunday 3 November 2013

MTAJI WA NCHI MASIKINI NI WATU WAKE WENYEWE!- MAGGID MJENGWA



Ndugu zangu,
Zamani sana kule kijijini kwetu Nyeregete wenyeji walibuni ushirikiano katika kilimo. Waliita ' mgowe'. ...
Msimu wa kilimo ukiwadia hutokea ndugu, jamaa na marafiki wa mwenye shamba wakakusanyika. Kwa pamoja walishiriki kulima shamba la mwenzao. Kazi hiyo ilienda haraka na kwa ufanisi. Siku nyingine walihamia kwa mwingine. Ni utaratibu tu waliojiwekea wa kuchangiana nguvu kwenye jambo la maendeleo.
Na leo nchi yetu iko kwenye mgogoro wa elimu. Hatua mbali mbali zinachukuliwa kujaribu kuutatua mgogoro huu. Tumeona juzi hapa , kuwa mabadiliko makubwa yamefanyika kuhusiana na mitihani, na Daraja la Sifuri limefutwa.
Lakini, tufike mahali tukubaliane kama taifa, kuwa bado hatujawekeza vya kutosha kwenye elimu. Ni tofauti na miaka ili ya baada ya Uhuru.
Pendekezo langu la moja kwa moja; kama taifa, tuanzishe sasa kampeni ya kuchangia shilingi moja tu kwa elimu. Kwamba kila mwenye kupiga simu, basi, akatwe shilingi moja tu , na kiasi hicho kiingizwe moja kwa moja kwenye mfuko wa kuchangia elimu.
Kwa idadi kubwa ya watumiaji wa simu waliopo na wanaoongezeka kila kukicha, kuna uwezekano mkubwa wa kupatikana fedha nyingi kuwawezesha Watanzania kusoma bure na kwa elimu bora kuanzia chekekechea hadi Chuo Kikuu. Na hapo tutakuwa tumejitahidi sana kupunguza matabaka katika jamii. Hapa Makabwela watakuwa wamejichangia katika jambo lao la maendeleo. Na hakika wengi wako tayari, hata kesho.
Maana, inatokea siku hizi kuwaona baadhi ya wanafunzi wa vyuo vikuu, na hasa watoto wa Makabwela, wakidhalilika kwa kulazimishwa kufunga virago kurudi makwao. Ni kwa kuwa hawana sifa za kupata mikopo. Kwamba hawakufaulu kwa kiwango cha daraja la kwanza kama ni wavulana, na daraja la kwanza au la pili kama ni wasichana.

Hapa haki ya kupata elimu tunaipa madaraja. Ni kwanini mtoto wa Kabwela mwenye sifa ya kujiunga na elimu ya juu asiwe na haki ya kupata mikopo ya elimu?!
Mwandishi Ngugi wa Thiong'o alipata kusema; Ukitaka kuelewa hali ya baadaye ya nchi itakavyokuwa, basi, angalia hali za vijana wa nchi hiyo kwa wakati uliopo.
Nami nitaongezea hapo alipoishia Ngugi, kwa kusema, na ukitaka kuelewa hali ya baadae ya nchi itakavyokuwa, basi, angalia hali za akina mama wake vijijini. Angalia pia hali za watoto wa akina mama hao.
Na tujiulize, je, vijana wetu leo wako katika hali gani? Je, akina mama wa leo wa vijijini na watoto wao wako katika hali gani?
Maana ni ukweli, kuwa karibu asilimia 84 ya Watanzania wanaishi vijijini. Na huko ndiko waliko akina mama wengi na watoto. Na akina mama wanabaki kuwa ndio mihimili halisia ya familia nyingi za vijijini. Hivyo basi, ni mihimili ya nchi. Na nimepata kuandika, kuwa ukitaka kuujua moyo wa nchi, nenda vijijini.
Swali, je, akina mama wa vijijini tunawajengee misingi gani ya kujikwamua kutoka katika hali zao duni walizo nazo sasa?
Jibu; ni kwa kupitia elimu bora kwa watoto wao.
Hivyo, na tuwe Wazalendo na Waaminifu kwa Nchi yetu tuliyozaliwa na tunayoipenda. Na tuamini pia, kuwa kama mtaji wa masikini ni nguvu zake mwenyewe, basi, mtaji wa Nchi Masikini ni Watu Wake Wenyewe.
Watanzania tuwe tayari sasa kuchangia shilingi moja ya kupigia simu, kwa Maendeleo ya Elimu. Hivyo basi, kwa Maendeleo ya Nchi Yetu. INAWEZEKANA.
Ni Neno la Leo. Maggid Mjengwa. Iringa.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!