Sunday, 3 November 2013

MHADHIRI WA CHUO CHA ELIMU YA BIASHARA JIJINI DSM, APAMBANA NA MAJAMBAZI YALIYOMVAMIA NYUMBANI KWAKE, AFANIKIWA KUUA JAMBAZI MOJA



MHADHIRI wa Chuo cha Elimu ya Biashara Dar es Salaam (CBE), Emmanuel Mwakyusa amefanikiwa kuwasambaratisha majambazi saba aliopambana nao nyumbani. Majambazi hao walimvamia nyumbani kwake eneo la Pugu jijini Dar es Salaam, ambapo alifanikiwa kumuua mmoja, kati ya wawili aliowajeruhi.
Tukio hilo lilitokea jana saa 8:30 usiku. Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala, Marietha Minangi alithibitisha kutokea kwa tukio hilo.
Alisema Mwakyusa aliwajeruhi majambazi wawili kwa risasi, ambapo mmoja alikufa na mwingine alifanikiwa kukimbia. Majambazi hao walimvamia Mwakyusa kwa lengo la kuiba mali nyumbani kwake.
Hata hivyo, hawakufanikiwa kupora mali yoyote baada ya wawili hao kujeruhiwa, hivyo wengine kukimbia. Kamanda Minangi alisema tayari watuhumiwa watatu, wameshakamatwa na upelelezi unaendelea ili kuwakamata wengine, waliohusika katika tukio hilo.
"Ni kweli tukio hilo limetokea na anadai walikuwa saba na mmoja alikuwa na bunduki, yeye pia alikuwa na silaha hivyo aliweza kujihami ambapo aliwajeruhi wawili mmoja kwa nje na mwingine aliyekuwa ameingia chumbani kwake," alisema Kamanda Minangi.
Alisema mmoja kati ya hao waliojeruhiwa, alikufa akiwa njiani kupelekwa hospitalini, maiti amehifadhiwa katika Hospitali ya Amana. Alisema majeruhi mwingine, alikamatwa asubuhi wakati amekwenda kuomba Fomu Maalumu ya Matibabu ya Polisi (PF3) katika kituo cha Polisi Gongo la Mboto.
"Alipofika kuomba PF3 alidanganya kuwa ameporwa pikipiki na majambazi ambao walimjeruhi, lakini alitiliwa shaka na baada ya kuhojiwa zaidi alikiri kuhusika katika tukio hilo na akawekwa chini ya ulinzi, wengine wawili walikamatwa katika maeneo tofauti," aliongeza.
Kamanda Minangi alisema mahojiano yanafanyika kwa hao waliokamatwa, ili kubaini wengine waliohusika ili pia waweze kukamatwa na sheria kuchukua mkondo wake.
Alisema katika tukio hilo, Mwakyusa na familia yake hawakujeruhiwa wala kupata matatizo yoyote kutoka kwa majambazi hao.
Akizungumza kwa njia ya simu na gazeti hilo, Mwakyusa alisema,"Wakati wameshaingia ndani walikuwa wanajiita majina yenye vyeo sawa na vile vya jeshi au polisi. Walikuwa wanaitana komandoo, kamanda na mengine ambayo ni sawa na vyeo"

HABARI LEO.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!