Friday 18 October 2013

WANAFUNZI WAWILI WA KIKE WA SHULE YA SEKONDARI BUNJU WAFA MAJI WAKATI WAKIOGELEA BAHARINI..

 

Wanafunzi wawili wa kike mkoani Dar es Salaam wamefariki dunia baada ya kuzama wakati wakiogelea baharini.

Wanafunzi hao wa kidato cha pili katika Shule ya Sekondari Wasichana ya Bunju, Manispaa ya Kinondoni, jijini Dar es Salaam, walifariki dunia juzi wakati wakisherehekea kumaliza mitihani yao ya kujiunga na kidato cha tatu.



Tukio hilo lilitokea katika ufukwe wa Ununio katika manispaa hiyo, baada ya marehemu pamoja na wanafunzi wenzao kufika huko kwa ajili ya kuogelea ikiwa ni sehemu ya kushangilia baada ya kumaliza mitihani.

Shuhuda wa tukio hilo, ambaye hakutaka jina lake litajwe, alisema aliwaona polisi wakifika eneo hilo kuchukua miili ya watoto hao baada ya ajali.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Camilius Wambura, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kuwataja waliofariki kuwa ni Clara Emanuel na Salama Mohamed, ambao alisema walikuwa wanasoma kidato cha pili katika Shule ya Sekondari ya Bunju.

Alisema wanafunzi hao baada ya kufika katika ufukwe huo wakiwa na wenzao, walianza kuogelea, lakini walizidiwa na maji na kuzama na kwamba, waliopolewa na mvuvi wa samaki wakiwa wamekufa.

Kamanda Wambura alisema baada ya mvuvi huyo kuwaopoa baharini, alikwenda kutoa taarifa polisi na kwamba, askari walifika eneo hilo na kuwachukua marehemu na kwenda kuwahifadhi katika Hospitali ya Mwananyamala.

Alisema wazazi wa marehemu wameshapatikana kufuatia jitihada za kuwatafuta zilizofanywa na polisi.


No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!