Saturday, 19 October 2013

UMOJA WA MATAIFA WAIPONGEZA TANZANIA KWA , AMANI , ULINZI NA USHIRIKIANO MZURI.

 Alberic Kacou

 

SHIRIKA la Umoja wa Mataifa (UN) limeipongeza Tanzania kwa ushirikiano mzuri katika amani na ulinzi, hasa katika uamuzi wake wa kuchangia katika vikosi vya kulinda amani nchini Kongo.

Mratibu Mkazi wa Shirika hilo, Alberic Kacou, alisema hayo jana Dar es Salaam. Alisema hayo wakati akitangaza kuanza kwa wiki ya maadhimisho ya miaka 68 kwa shirika hilo, iliyoanza na matukio mbalimbali.

Kilele cha maadhimisho hayo kitakuwa Alhamisi ijayo. Kacou aliipongeza Serikali kwa kuonesha ushirikiano wa dhati haswa katika suala la ulinzi na amani. Alitoa pole kwa askari waliopoteza maisha katika vikosi hivyo wakati wakilinda amani.

“Tunashukuru sana Serikali inayoongozwa na Rais Jakaya Kikwete kwa kushirikiana katika suala la ulinzi na amani,” alisema Kacou. Aliongeza kuwa katika sherehe hizo za miaka 68, UN itajadili pia miradi mbalimbali ambayo imekuwa ikitekelezwa na shirika hilo hapa nchini.

Kuhusu maadhimisho hayo, alisema UN imekuwa ikiendesha majadiliano kimataifa yenye kuonesha ni dunia ya aina gani wananchi wanaihitaji, haswa baada ya mwaka 2015 kwa kuangalia masuala ya afya, elimu, ajira, mazingira, utawala bora, migogoro kwa nchi mbalimbali na nishati.

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Rajab Gamaha, alisema katika kuadhimisha miaka hiyo, Tanzania itashirikiana na UN kwa kuendesha shughuli mbalimbali, ikiwa ni pamoja na kuwa na mjadala wa wazi utakaohusu masuala ya maendeleo, mafanikio na changamoto zinazoikabili Tanzania.

Alitaja mambo mengine yatakayofanyika kuwa ni kujadili namna ya kuwaandaa vijana kwa ajili ya kesho ili Tanzania iweze kuwa yenye neema zaidi, hasa kwa kuzingatia kaulimbiu ya ‘Tanzania kesho tunataka’.

CREDIT HABARI LEO.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!