Pages

Saturday, 19 October 2013

PINDA-VIONGOZI WAFUNZWE WABADILI MWELEKEO





WAZIRI Mkuu Mizengo Pinda amesema kuna haja ya taasisi za mafunzo ya uongozi za China na Tanzania kuandaa kozi zenye kufaa kwa makundi fulani ya viongozi ambazo zitasaidia kubadili mwelekeo wao na utendaji wao wa kazi hasa katika masuala yanayohusu sekta binafsi.
Amesema taasisi hizo zinapaswa kuwa na uelewa mkubwa kuhusu ushirikiano wa pamoja baina ya sekta binafsi na za umma (PPP), zinapaswa kujua faida za ushirikiano huo na zinapaswa kubainisha ni sekta zipi zinapaswa kutekeleza mpango huo wa ushirikiano.
Ametoa kauli hiyo jana wakati akifungua mafunzo ya siku 14 kwa maofisa 20 kutoka idara na taasisi za serikali ya Tanzania yanayoendeshwa kwa pamoja baina ya Chuo cha Uongozi cha China na Taasisi ya Uongozi ya Tanzania.
Mafunzo hayo ni sehemu ya mpango wa Serikali kuboresha utendaji wa Maeneo ya Uzalishaji kwa Mauzo ya Nje (EPZ) yameanza leo kwenye Chuo cha Uongozi cha China (China Governance Academy), jijini Beijing, China.
Alisema Tanzania imefanya maamuzi ya kutumia ushirikiano wa pamoja baina ya sekta binafsi na za umma (PPP) kama njia ya kukuza na kuendeleza miundombinu, kuhamisha ujuzi na teknolojia pamoja na ujenzi wa viwanda.
“Ni muhimu taasisi zetu hizi mbili zikatambua jambo hili na kuchangia kwa juhudi zote ili kuhakikisha kuwa linafanikiwa,” alisema.
Waziri Mkuu ambaye yuko katika siku ya tatu ya ziara ya kikazi yake ya siku tisa kwa mwaliko wa Serikali ya nchi hiyo, alitembelea kiwanda cha aluminium cha China CHINALCO) na kiwanda cha kutengeneza zana za kijeshi ambako alionyeshwa bidhaa mbalimbali zinazozalishwa na viwanda hivyo.
Wakati huo huo, Waziri Mkuu Mizengo Pinda amemwomba Waziri Mkuu wa China, Li Keqiang kuhamasisha kwa nguvu kampuni na wafanyabiashara wa China kuwekeza nchini Tanzania kutokana na kuwepo fursa nyingi ambazo hazijapata wawekezaji.
Maeneo ambayo Pinda aliyataja kuwa wanahitaji uwekezaji wa haraka na wa nguvu ni kwenye eneo la ujenzi wa viwanda vya ngozi na viatu, uwekezaji katika usindikaji wa maua, mboga na matunda, ujenzi wa viwanda vya nguo pamoja na ujenzi wa viwanda vya maziwa.
Eneo lingine ni ujenzi wa viwanda vya saruji na mbolea, ujenzi wa viwanda ambavyo vitakuwa kwenye maeneo huru ya uchumi (EPZ) na Maeneo Maalumu ya Uchumi (SEZ) pamoja na uwekezaji katika ujenzi wa vituo vya biashara na usafirishaji.
Pinda aliainisha maeneo hayo katika mazungumzo yake na mwenyeji wake waziri mkuu wa China, Li Keqiang ambaye ndiye aliyemwalika kufanya ziara ya kiserikali nchini hapa.
Alisema ugunduzi wa gesi katika maeneo ya kusini mwa Tanzania ni jambo la kujivunia na akasema wanaiomba China isaidie katika eneo la teknolojia na uchimbaji wa gesi yenyewe ili iweze kuwa yenye manufaa kwa nchi. Pia aliishukuru China kwa kukubali kujenga bomba la gesi kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam.

No comments:

Post a Comment