Mahakama ya Wilaya Singida imewahukumu watu wanne kutumikia vifungo vya miaka 120 jela kwa kuteka gari lililokuwa likisafirisha maiti kutoka mkoani Morogoro kwenda Musoma mkoani Mara na kupora waombolezaji kompyuta na fedha.
Waliohukumiwa vifungo hivyo kila mmoja miaka 30 jela ni Hamis Ali (23), Hamisi Issa (33); Khaldi Hamis (21) na Abubakari Jumanne (26), wakazi wa Kisaki Manispaa ya Singida.Mshtakiwa wa kwanza Iddi Omari (38), aliachiwa huru baada ya mahakama hiyo kukosa ushahidi wa kumtia hatiani. Akisoma hukumu hiyo, Hakimu Mfawidhi wa mahakama hiyo, Flora Ndale, alisema ushahidi uliotolewa na upande wa mashtaka bila kuacha shaka umethibitisha washtakiwa hao walitenda kosa hilo.
Awali, Mwendesha Mashtaka,Sajini, Godwel Lawrence, alidai kuwa Desemba 6, mwaka 2012, saa 7:30 mchana, eneo la Kisaki, washtakiwa hao waliteka gari lenye namba za usajili SU 37012 aina ya Toyota Land Cruiser mali ya serikali lililokuwa likiendeshwa na Kalistus Malipula, wakati limebeba mwili wa Munchari Lyoba aliyefariki dunia akiwa mwanafunzi mwaka wa tatu Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine (Sua) kwa ajili ya kuusafirisha kutoka Morogoro kwenda Musoma mkoani Mara kwa maziko
Alidai baada ya washtakiwa hao kuteka gari hilo waliwapora waombolezaji vitu mbalimbali zikiwamo kompyuta mpakato, simu za mkononi na fedha taslim zaidi ya Sh. milioni 8.7.
Alidai pia walivunja jeneza na kuufanyia upekuzi mwili wa marehemu huyo kwa kuchana sanda wakidhani kulikuwa na fedha zilizofichwa.
Kwa upande wao, washtakiwa hao waliiomba mahakama iwapunguzie adhabu kutokana na kutofanya kosa hilo, umri wao kuwa mdogo na wanategemewa na familia zao.
Ombi hilo lilipingwa na mwendesha mashtaka na kuiomba mahakama kutoa adhabu kali ili liwe fundisho kwa watu wengine wenye tabia kama hiyo.
Hakimu Ndale alisema kosa lililofanywa na washtakiwa hao ni la kinyama na lisingeweza kuvumilika katika jamii, hivyo ili liwe fundisho kwa wote wanaofikiria kufanya vitendo vya kinyama kama hicho, anawahukumu kila mmoja kutumikia kifungo cha miaka 30 jela.
Hakimu Ndale alisema kosa lililofanywa na washtakiwa hao ni la kinyama na lisingeweza kuvumilika katika jamii, hivyo ili liwe fundisho kwa wote wanaofikiria kufanya vitendo vya kinyama kama hicho, anawahukumu kila mmoja kutumikia kifungo cha miaka 30 jela.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment