Friday, 25 October 2013

JE WAJUA HISTORIA YA MAKUMBUSHO YA VITA VYA MAJI MAJI SONGEA


 Maandishi yanampa msomaji picha ya halisi ya historia ya Makumbusho ya maji maji yaliyopo katika mji wa Songea kusini mwa Tanzania.
Mkoa wa Ruvuma unapakana na nchi ya Msumbiji kwa upande wa kusini,Kasikazini mkoa huu unapakana na mkoa wa Morogoro,Kaskazini-Magharibi mkoa wa ruvuma unapakana na mkoa wa iringa.Magharibi mkoa huu unapakana na nchi ya Malawi na kwa upande wa mashariki kuna mikoa ya Lindi na Mtwara.

Historia ya Makumbusho haya inahusu vita ya Maji Maji vilivyo tokea kati ya mwenzi julai.1905 mpaka Agosti 1907.Vita hivi vilianza katika vilima vya Umatumbi Kaskazini mwa mji wa Kilwa mnamo mwazi Julai mwaka 1905.
Waanzilishi wa awali wa vita hii walikuwa ni Wamatumbi chini ya uhamasishaji wa Mganga wa jadi/Nabii aliye julikana kwa jina la Kinjeketile.Vita hivi vilienea kama moto katika nyasi kavu na kusambaa katika makabila ya Wamwera,Wangindo,Wapogoro,Wangoni,Wabena,Wasangu na wengineo. Watu hawa walipigana kupinga kukandamizwa na kulazimishwa na wakoloni wa Kijerumani namna ya kuishi,mazao ya kuzalisha na nani wa kumtumikia.
 Picha ya Askari wa Kijerumani

Jina la vita hivi lilitokana na imani ya matumizi ya dawa iliyochanganywa na Maji,punje za mahindi na mtama zilizosadikiwa kuwa zitampa mpiganaji kinga ya kutodhurika kwa shambulio la risasi za majeshi ya Wajerumani.Inakadiriwa watu 75,000 walipoteza maisha yao ukanda wa kusini mwa Tanzania baada ya vita. Katika eneo la Ruvuma inakadiriwa kuwa zaidi ya watu 1,000 walipoteza maisha yao.

Baada ya vita viongozi na askari walioshiriki katika vita walikamatwa na kuhukumiwa kunyongwa mpaka kufa.Tarehe 27 February 1907 ilikuwa siku ya masikitiko makubwa kwa watu wa Ruvuma  ambapo kadri ya watu 60 walinyongwa kwa sababu ya kushiriki katika vita. Mashujaa hawa walinyongewa nyuma ya eneo ambalo leo hii linajulikana kama “Songea Club”. Baada ya kunyongwa miili yao ilizikwa katika kaburi la halaiki,lililoandaliwa na wafungwa kwa muda wa miezi miwili. Siku tatu baadaye Chifu Songea alinyongwa na kuzikwa katika kaburi lililoandaliwa na kaburi la halaiki.
Hili ndilo Kaburi la halaiki walipozikwa mashujaa wa vita vya Maji Maji , watu waliozikwa hapa ni 66
 
Eneo walilozikwa mashujaa hawa limekuwa eneo muhimu.

Tukio hili lilikuwa la huzuni sana kwa watu wetu hivyo watu hawakulizungumza kwa kitambo kirefu. Baada ya uhuru (1961) Baadhi ya wazee walianzisha harakati za kuwakumbuka mashujaa hawa. Walianza  kufanya maombi yao na maadhimisho katika eneo lililo karibu na eneo walilonyongewa wapiganaji hao.Shughuli hizi zilifanyika katika nyumba ya Padre Chengula.


Wazo la kuwa na maadhimisho ya Kitaifa lilianzishwa na kamati ya wazee wa kingoni.Walitoa taarifa kwa Mkuu wa mkoa Bw Martin Haule aliyekuwa ameteuliwa wakati huo.Baadhi ya wazee waliokuwa katika kamati hii ni pamoja na Xavery Zulu,Padrea Chengula,Daudi Mbano,Ali Songea Mbano,Agatha Shawa,Alana Mbawa,Mwl Duwe,Shaibu Mkeso na Daniel Gama.


 Baada ya kuwasilishwa wazo hili kwa Mheshimiwa Martin Haule,alichukua hatua za dhati katika kulishughulikia jambo hili.Hatua ya kwanza ilikuwa kutambuwa eneo ambalo mashujaa hawa walizikwa.

Eneo hili walipozikwa mashujaa lilitambuliwa na Bw Jumbe Darajani ambaye alishuhudia tukio la kunyongwa kwa wahenga hawa(wakati wa utoto wake). Alama iliyotumika kufahamu eneo hili ilikuwa ni mti mmoja uliojulikana kwa jina la CHIKUNGUTI.Baada ya kutambuwa eneo hili mheshimiwa Haule alifanya uchimbuzi na kupata baadhi ya mifupa.

 Kaburi la Songea Mbano ambaye alizikwa peke yake na jina la Mji wa Songea limetokana na jina lake



Kabla ya Bwana Haule kukamilisha kazi hii alihamishiwa mkoa wa Ruvuma mwaka 1964.Wazo hili la kuwaenzi wahenga hawa liliibuka tena mwaka 1979 wakati Bw Laurence Gama alipoteuliwa kuwa Mkuu wa mkoa wa Ruvuma.Aliendelea na jitihada za kutekeleza wazo hili.  Alianza kuhamasisha na kutafuta Fedha kwa ajili ya ujenzi wa makumbusho kwa kushirikiana na wazee wa Ruvuma na Wananchi wengine ujenzi wa jengo la makumbusho ulianza na kukamilika mwaka 1980.


Pamoja na kukamilisha ujenzi wa jengo hili pia zilijengwa sanamu katika eneo la mbele ya jengo.sanamu hizi zinajumuisha sanamu ya Askari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania,Mwl J.K Nyerere na sanamu 12 za machifu wa kingoni.Lakini kwa sasa sanamu ya hayati Mwl J.K Nyerere imetolewa baada yakuonekana haina kiwango cha juu hivyo inaandaliwa sana upya ili iweze kuwekwa upya.Kazi ya kutengeneza sanamu hizi ilifanywa na msanii mmoja huko Arusha.


Vifaa vya awali katika Makumbusho haya vilikusanywa na Mheshimiwa Laurence Gama, Padri Chengula na baadhi ya wazee. Vifaa vilivyokusanywa vilijumuisha silaha zilizotumika wakati wa vita vya Maji Maji kama vile Chikopa(Ngao), Chibonga(Rungu),Chinjenje(Kishoka), pia baadhi ya viti vilivyotumiwa na Chifu Mputa, Vifaa vya ndani na nguo za magome ya Miti.


Kuanzia mwaka 1980 baraza la wazee lilianza kuadhimisha maombolezo ya mashujaa walionyongwa kila ifikapo tarehe 27 Februari ya kila Mwaka. Makumbusho haya yalifunguliwa rasmi tarehe 7 Julai 1980.Kuanzia hapo makumbusho haya yaliendelea kutoa huduma chini ya usimamizi wa Mkoa wa Ruvuma na wazee wameendelea kufanya maadhimisho ya kila siku ya mashujaa katika eneo la Makumbusho haya ila mwaka.

Baadhi ya wazee ndio ambao wamekuwa wakitoa maelezo kwa wageni wanaotembelea makumbusho haya. Tarehe 1 September 2005 makumbusho haya yalikabidhiwa kwa Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Miaka 100 ya vita vya Maji Maji iliadhimishwa kitaifa katika Makumbusho haya tarehe 27 Februari 2006 na yalizinduliwa rasmi na Rais wa Tanzania Mhe. Jakaya Kikwete

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!