Wednesday, 30 October 2013

ALIYEUAWA MGODINI AZIKWA







MGODI wa dhahabu wa Geita (GGM) uliopo mjini Geita, umegeuka shubiri kwa baadhi ya wakazi wa wilaya hiyo kufuatia walinzi wake kudaiwa kugeuka kuwa wakatili wa kushambulia watu na kuwasababishia vifo.

Hali hiyo imesababisha matukio ya watu kufa wakiwa ndani ya mgodi huo kuongezeka baada ya mtu mwingine, Zacharia Tabaro (36), mkazi wa Mtaa wa Ibisabageni mjini Sengerema mkoani Mwanza kudaiwa kufa kwa kushambuliwa na walinzi wa mgodi huo.
Mwanaume huyo inasemekana alishambuliwa na walinzi kwa vitu vyenye ncha kali pamoja na mawe na kusababisha kufariki dunia.
Tukio hilo limetokea usiku wa Oktoba 16, mwaka huu baada ya marehemu kudaiwa kuingia mgodini humo kwa muda usiojulikana kwenda kuchukua mawe yanayosadikika kuwa na dhahabu maarufu kwa jina la magwangala.
Mmoja wa ndugu wa marehemu, Mengi Paulo alisema: “ Tabaro aliondoka Mugusu mjini Geita katika mazingira ya kutatanisha na juhudi za kumtafuta zilifanyika bila mafanikio.”
Aliongeza kuwa Oktoba 16, mwaka huu majira ya alfajiri walipata taarifa kwa njia ya simu kutoka kwa baadhi ya wafanyakazi wa mgodi huo kwamba kuna mtu alikufa mgodini.
Alisema baada ya taarifa hiyo, saa 3 asubuhi waliingia mgodini humo na kuikuta maiti ya ndugu yao ikiwa na jeraha kubwa juu ya paji la uso lililotokana na kupigwa kwa mawe huku kifuani akiwa amewekewa jiwe zito.
Alipoulizwa kama ndugu yao ameuawa na walinzi wa mgodi huo, Paulo alisema inawezekana kutokana na kwamba walinzi wanapowaona watu mgodini humo wakiwa wameingia bila taratibu, huwapiga kwa mawe.
“Matukio ya watu kupigwa siyo tukio la kwanza mara nyingi yanajitokeza, watu wengi wamepoteza maisha ndani ya mgodi huo,” alisema Paulo ambaye ni mpwa wa marehemu.
Ofisa Habari wa Mgodi wa Geita (GGM), Tenga Birri Tenga, alipotafutwa kwa njia ya simu kuzungumza kama walinzi wa mgodi huo wamehusika katika  mauaji ya mtu huyo alisema taarifa hizo siyo za kweli.
“Siyo kweli ndugu yangu, huyo mtu hajauawa na walinzi isipokuwa wao wenyewe wachimbaji wadogo walimpiga na baada ya kumuua walichukua mwili wake na kuutupa mgodini.”
Kaimu Kamanda wa Polisi mkoani Geita, Pundensiana Protas alipotafutwa kuzungumzia tukio hilo kwa njia ya simu baada ya kuwa nje ya ofisi, simu yake ilipokelewa na mlinzi wake ambaye alidai kwamba alikuwa kwenye kikao.
Hata hivyo, mwili wa marehemu ulichukulia na polisi kutoka mgodini humo na kupelekwa katika Hospitali ya Wilaya ya Geita kwa ajili ya uchunguzi, baadaye ndugu wakapewa na kwenda kuuzika Mwanza.
Takwimu zinaonyesha kuwa watu zaidi ya 30 wamekufa ndani ya mgodi huo katika kipindi cha kuanzia Januari mwaka jana hadi Septemba mwaka huu.
chanzo:globalpublishers

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!