Sunday, 22 September 2013

WACHIMBAJI TANZANITE WAFA KWA KUKOSA HEWA MGODINI USIKU...


Eneo la machimbo ya Tanzanite.
Watu wawili ambao ni wachimbaji wadogo wa madini ya tanzanite katika Mji mdogo wa Mirerani wilayani Simanjiro, Manyara wamekufa wakiwa ndani ya mgodi baada ya kukosa hewa.

Akithibitisha vifo hivyo, Kaimu Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Manyara, Kamishna Msaidizi, Mussa Marambo alisema vilitokea Septemba 20 mwaka huu saa 4 usiku.
Kamanda Marambo aliwataja wachimbaji waliokufa kuwa ni Amos Goodluck (23), mkazi wa Kibaoni, King'ori wilayani Arumeru, Arusha na Baraka Ramadhan (24), mkazi wa Songambele Mji mdogo wa Mirerani wilayani hapa.
"Wachimbaji hao wawili walifariki dunia wakiwa wanafanya kazi kwenye mgodi wenye namba PML  0003337 uliopo kitalu D unaomilikiwa na Boniface John Mgalla (51) mkazi wa Mbuguni wilayani Arumeru mkoani Arusha," alisema Kamanda Marambo.
Alisema chanzo cha tukio hilo ni wachimbaji hao kuingia kwenye mgodi huo na kwenda kufanya kazi katika sehemu ambayo haitumiki kufanyika kazi hivyo, wakakosa hewa na kuishiwa nguvu na hatimaye kufia ndani ya mgodi.
Aidha, alisema miili ya marehemu hao imehifadhiwa kwenye Hospitali ya Mkoa wa Arusha ya Mount Meru, kwa uchunguzi zaidi na bado polisi wanaendelea na uchunguzi wa tukio hilo.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!