Saturday, 21 September 2013

VISA ZA KIPAUMBELE ZAANZISHWA

Embassy in Kenya - Nairobi - British



 Ili kuimarisha biashara, Ubalozi wa Uingereza nchini umesema, kuanzia sasa Watanzania wanaotaka huduma za viza kwa ajili ya kwenda nchini humo wanaweza kupata huduma hiyo katika kipindi cha muda mfupi kutokana na  kuanzishwa kwa kile kinachoitwa ‘viza za kipaumbele’.
Huduma hiyo ambayo pia imeanza kutumika katika nchi nyingine za Uganda na Kenya inaelezwa kuwa ni moja ya mkakati wa Serikali ya Uingereza kuongeza kasi ya ushirikiano na uwekezaji nchini.
Balozi wa Uingereza nchini, Dianna Melrose alisema uhusiano wa kibiashara baina ya nchi hizi mbili umeimarika zaidi katika miaka ya hivi karibuni hivyo kuanzishwa kwa huduma hiyo mpya kutasaidia kuharakisha kufikia malengo ya kibiashara kwa pande zote.
“Huduma hii ya kipaumbele itahakikisha maombi ya viza yanafanyiwa kazi ndani ya siku tano na mwombaji atatakiwa kulipia kiasi cha Sh250,000,” alisema Balozi Melrose.
Hata hivyo, alifafanua kuwa, pamoja na kuanzishwa kwa huduma hiyo mpya, zoezi la utoaji viza litaendelea kufanywa kwa kufuata sheria za kawaida za uhamiaji.
Viza hizo za kipaumbele zinatazamiwa kutolewa katika makundi mbalimbali ikiwamo wafanyabiashara, wanafunzi na wale wanaokwenda kwa matembezi ya kawaida.
Alisisitiza kuwa viza za kipaumbele zina lengo la kufanya mchakato wa maombi kuwa wa kasi zaidi hasa kwa wafanyabiashara pamoja na wengine ambao watahitaji kufanya maombi ndani ya muda mfupi.
“Tunafanya hivi kutokana na maombi ya wengi, pia kutokana na kukua kwa uhusiano wa kibiashara ili kuleta maendeleo na ajira kwa Watanzania na Waingereza,” alisema Balozi Melrose. 
Kuhusu utoaji viza kupitia ubalozi wake Nairobi, Kenya, Balozi Melrose alisema “Tunafanya hivyo ili kuwa na ufanisi mzuri wa kazi na hakuna upendeleo wowote.”

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!