Thursday, 19 September 2013

TANZANIA KUSHIKA NAFASI YA NNE KWA UZALISHAJI WA CHUMA


NGAPEMBA
 Na Hassan Silayo na Fatma Salum , MAELEZO
18/0/2013 Tanzania inatarajia kuwa mmoja wa wazalishaji wakubwa wa chuma barani Afrika kwa kuzalisha tani milioni moja kwa mwaka pindi uzalishaji wa madini hayo utakapoanza mwaka 2018/19 katika eneo la Liganga wilayani Ludewa.
Hayo yamebainishwa na Meneja Uhusiano na Mawasiliano wa Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC) Abel Ngapemba wakati akizungumza na waandishi wa habari  jijini Dar es Salaam leo.
Alisema mradi huo wa uzalishaji chuma utakaotekelezwa chini ya kampuni ya Tanzania China Mineral Resources Limited (TCIMRL), ambayo ni kampuni ya ubia kati ya Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC) na Shirika la Sichuan Hongda Group (SHG) ya China utaenda sambamba na uzalishaji wa madini ya Titanium na Vanadium.
“Mradi huo ukikamilika tutaweza kuzalisha tani milioni 219 za chuma ambazo zitadumu kwa zaidi ya miaka 70, na madini mengine yatakayotokana na mgodi huo ni Titanium tani 175,400 kwa mwaka na Vanadium tani 5,000 kwa mwaka”. Alisema Ngapemba.
Aidha Ngapemba alisema kuwa uzalishaji huo utaiwezesha Tanzania kushika nafasi ya nne ikizifuatia nchi za Afrika Kusini inayozalisha bidhaa za chuma tani milioni 8.5 kwa mwaka, Misri tani milioni 8.0 na Libya tani milioni 2.0 kwa mwaka.
Mradi huu ni moja ya miradi miwili iliyopo katika mkataba kati ya NDC na SHG uliotiwa saini Septemba 21, 2011 ya uanzishwaji wa mgodi wa makaa ya mawe na ujenzi wa kituo cha kufua umeme wa megawati 600 katika eneo la Mchuchuma.
 Miradi  mingine ni pamoja na ujenzi wa  msongo wa umeme wa kilovoti 220 kati ya Mchumchuma na Liganga, na uanzishwaji wa mgodi wa chuma pamoja na  ujenzi wa kiwanda cha kuchenjua chuma , kiwanda cha kuzalisha bidhaa za chuma na ujenzi wa barabara kati ya Mchuchuma na Liganga.
Chuma kinachozalishwa duniani ni takribani tani bilioni 1.55 kwa mwaka, mzalishaji mkubwa ikiwa ni China inayotoa tani milioni 711 kwa mwaka ambayo ni sawa na asilimia 46 ya chuma chote kinachozalishwa duniani.
Miradi hii itakayogharimu Dola za Kimarekani bilioni 3 inatarajiwa kuliingizia Taifa mapato ya Dola bilioni 1.7 kwa mwaka itakapoanza uzalishaji wake. 

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!