Saturday 21 September 2013

TAARIFA MAALUM KWA UMMA KUTOKA WIZARA YA MAMBO YA NDANI



 


Taarifa Maalum Kwa Umma Kutoka Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchini Juu ya Operesheni Kimbunga na Usakaji Wahalifu Katika Mikoa ya Kagera, Kigoma na Geita ambao kwa kiasi kikubwa umechangiwa na kuwepo kwa wahamiaji haramu kutoka nchi jirani



JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

WIZARA YA MAMBO YA NDANI YA NCHI
 





Simu:  +255-22-2112035/40
        S.L.P.  9223
Nukushi:  +255-2122617/2120486
Barua Pepe:  ps@moha.go.tz
       Dar es Salaam
Septemba 19,2013

---

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete Julai 29, 2013 aliagiza kufanyika operesheni maalum iliyopewa jina la  Operesheni Kimbunga  yenye lengo la kuondoa uhalifu katika mikoa ya Kagera, Kigoma na Geita ambao kwa kiasi kikubwa umechangiwa na kuwepo kwa wahamiaji haramu kutoka nchi jirani.
 

Operesheni hii pamoja na kufanikiwa kuondosha nchini kwa lazima jumla ya wahamiaji haramu 7,819 kuanzia Septemba 6, 2013 hadi kufikia Septemba 17, 2013,   imeweza kushughulikia uhalifu na kufanikiwa kukamata majambazi wa kutumia silaha, majangili, mabomu ya kutupwa kwa mkono , bunduki za aina mbali mbali, Risasi, mitambo ya kutengeneza bunduki aina ya magobole, Sare za Jeshi la Wananchi wa Tanzania, na kibuyu cha maji cha Jeshi hilo.
 

 Jumla ya watuhumiwa wa ujambazi wa kutumia silaha 55 pamoja na mabomu ya kutupwa kwa mkono (8), silaha 47 zikiwemo bunduki aina ya SMG( 4), Shot gun (4), Bunduki aina ya Riffle (2), Bunduki aina ya Mark IV (1), Bunduki aina ya Gobole (37) zimekamatwa wakati wa operesheni Kimbunga hadi kufikia Septemba 17,2013 katika mikoa ya Kagera, Kigoma na Geita.
 

Aidha,   risasi (602) zilikamatwa zikiwemo Risasi (500) za bunduki ya aina ya SMG na SAR, Risasi (20) za bunduki aina ya Mark IV na risasi (82) za bunduki aina ya Gobole, fataki (8), mitambo ya kutengeneza magobole (2), misumeno ya kukata miti ( 9), Mbao (1,516), Magogo (86), na mkaa magunia (111).
 

Aidha, Watendaji wa Operesheni Kimbunga pia wamefanikiwa kukamata jumla ya majangili Watanzania (3), Vipande vya meno ya Tembo (2), Ngozi za wanyama mbali mbali wakiwemo  Nyati (1), Duma (1) na Swala (2). Pia walikamata nyama ya porini,  magunia ya bangi  (6), Gongo lita (86) na lami mapipa (10). 
 

 Wakati huo huo,  Ng’ombe 3,436  wamekamatwa  baada ya wafugaji haramu kutelekeza mifugo hiyo wakati walipozingirwa na timu ya operesheni kimbunga katika mikoa ya Kagera, Kigoma na Geita.
 

Kumekuwepo na tabia ya baadhi ya wamiliki wa mifugo kutoka nchi jirani ambao wengi wao ni matajiri na viongozi serikalini kuwatuma watumishi wao kuingiza mifugo katika ardhi ya Tanzania hususan kwenye hifadhi ya Taifa kwa ajili ya malisho na watumishi hao hupewa silaha kwa ajili ya kujihami wakiwa kazini.  
 

Mifugo imekuwa ikiharibu mazingira na kuleta migogoro ya ardhi katika mikoa hii.

Operesheni Kimbunga itahakikisha inawakamata wahalifu wote wanaotishia amani hususan katika mikoa ya Kagera, Kigoma na Geita. 
 

Aidha, wananchi ambao ni raia pamoja na Raia wenye asili ya nchi jirani wanaowakaribisha na kuwahifadhi wahalifu na wahamiaji haramu watakamatwa na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria. 
 

Mhamiaji haramu ni raia yeyote wa kigeni aliyeingia na kuishi nchini  bila kufuata utaratibu uliowekwa na  Sheria ya Uhamiaji namba 7 ya mwaka 1995.
 

Utaratibu chini ya Sheria hiyo unamtaka raia wa kigeni anayeingia nchini kuwa na Hati ya kusafiri, kuripoti katika vituo halali vya kuingilia nchini na kujaza fomu za uhamiaji za kuingia nchini.
 

Aidha, Raia wa kigeni anayehitaji kuishi nchini analazimika kuwa na hati za ukaazi itakayomruhusu kufanya shughuli iliyomleta mfano biashara,  matembezi, uwekezaji, Kusoma, matibau, kufanyakazi nakadhalika.
 

Operesheni Kimbunga inayoongozwa na Brigedia Jenerali Mathew Sukambi imeanza rasmi Septemba 6, 2013 baada ya kutoa muda wa wiki Mbili kwa wahamiaji wanaoishi nchini bila kufuata sheria kuondoka kwa hiari.



Taarifa hii imetolewa na  Zamaradi Kawawa, Kiongozi wa  Timu ya Habari na Mawasiliano ya Operesheni Kimbunga. Septemba 19, 2013, Biharamulo, Kagera. Kwa maelezo zaidi piga Simu namba 0754698856, Email; zamaradikawawa@yahoo.com

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!