
Benki ya Barclays tawi la Morogoro imekumbwa na kashfa
baada ya wafanyazi wake kwa nyakati tofauti kuchota kwenye akaunti fedha za
mteja wake Sh. milioni 399.8.
Wizi huo unadaiwa kufanywa kati ya Septemba 2012 hadi
April mwaka huu kwenye akaunti namba 0096000138 ya mteja huyo ambaye ni
wafanyabiashara maarufu wa mjini Morogoro.
Mfanyabishara huyo, Ajay Gokal, alisema alibaini wizi
huo mwishoni mwa mwaka jana baada ya kuona fedha katika akaunti yake zikipungua
siku hadi siku na kuamua kuomba taarifa ya fedha kwenye akaunti yake Novemba
mwaka jana na kubaini kuwapo kwa upungufu wa Sh. milioni 119 na kuamua kuomba
taarifa ya mwaka mzima.Gokal ambaye ni mfanyabiashara wa moja ya kampuni ya simu
ya mikononi, alisema baada ya kuomba taarifa ya mwaka alikuwa akizungushwa na
uongozi wa benki hiyo hali iliyomlazimu kwenda kufungua jarada katika kituo cha
polisi.
Alisema alilazimika kufanya hivyo kutokana na risiti za
wateja wake walizoingiza fedha katika akaunti yake kuonyesha kuna fedha
ziliingizwa, lakini kwenye akaunti hazionekani.
“Nina risti za benki hiyo kutoka kwa wateja wangu
niliowapa mzigo na kuniingizia fedha hizo, lakini nikienda kuangalia katika
akaunti hiyo sioni hizo fedha nikawafata wanipe taarifa za fedha wananizungusha
mpaka nikaenda kufungua jarada katika kituo cha polisi,” alisema
Gokal.
Alisema baada ya kufungua kesi maafisa wa Jeshi la
Polisi waliamuru uongozi wa benki kumpatia taarifa hizo kwa kuwa ni haki yake,
lakini cha kushangaza ilikuwa ikimpatia miezi miwili huku mingine
ikirukwa.
Alisema baada ya kupitia kumbukumbu hizo toka Novemba
mwaka jana hadi Aprili 13 mwaka huu, alibaini kuibiwa Sh. milioni
399.8.
Hata hivyo, alisema alipojaribu kuwasilina na uongozi
wa benki, ulidai kuwa suala hilo wanalishughulikia na kumshauri asilifikishe
suala hilo katika vyombo vya habari kwani haliwezi kupatiwa
ufumbuzi.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Faustine Shilogile,
alithibitisha kupata taarifa hizo. Alisema polisi ilianza kufanya uchunguzi
baada ya uongozi wa benki hiyo kudai kuwa risiti zilizotumika kuweka fedha
katika akaunti ya mteja huyo hawazitambui.
Kutokana na hali hiyo, jeshi hilo limewahoji
wafanyakazi wa benki hiyo na kuwashirikilia watatu kwa tuhuma hizo huku
uchunguzi zaidi ukiendelea na kwamba baada ya kukamilika jarada litapelekwa kwa
Mwanasheria wa Serikali ili kufunguliwa kwa mashtaka.
Meneja wa benki hiyo tawi la Morogoro, Angelo Mahembe,
alipotafutwa na nipaswe kupata ufafanuzi hakukubali wala kukataa. Hata hivyo,
alishauri watafutwe viongozi wa makao makuu kwa maelezo kuwa yeye siyo
msemaji.













No comments:
Post a Comment