Thursday, 18 April 2013

MAKALA MAALUM YA JUU USIYOYAJUA KUHUSU BI KIDUDE




Bi Kidude ni gwiji wa muziki katika Bara la Afrika. Jina lake halisi ni Fatuma binti Baraka.

Fatuma binti Baraka au Bi Kidude, alizaliwa katika kijiji cha Mfagimarigo Zanzibar katika familia ya watoto saba (7). Baba yake Mzee Baraka alikuwa ni mfanyabiashara wa nazi, zao ambalo ni la kutumainiwa sana Zanzibar. Bi Kidude anasema hafahamu tarehe halisi aliyozaliwa, isipokuwa anachojua ni kwamba alizaliwa wakati rupia ikitumika kama fedha, na vilevile ana hakika ni kabla ya Vita Kuu ya Kwanza ya Ulaya.

Bi Kidude anasema uimbaji aliuanza tangu alipokuwa na umri wa miaka 10 na alijifunza kutoka kwa msanii mkongwe na aliyetamba sana enzi hizo Sitti binti Saad.

Alipokuwa na miaka 13, alitoroka nyumbani kwao Zanzibar na kukimbilia Tanzania Bara, baada ya kulazimishwa kuolewa. Lakini alipokuwa kigoli wa kutosha kuolewa aliolewa ingawa ndoa hiyo nayo haikudumu kutokana na manyanyaso aliyokuwa akiyapata, hivyo aliamua kukimbilia kaskazini mwa Misri ikiwa ni katika miaka ya 1930, huko aling'ara sana katika fani yake ya uimbaji na uchezaji ngoma. Lakini ilipofika miaka ya 1940 aliamua kurudi nyumbani Zanzibar ambako aliendelea na shughuli zake uimbaji.



Mbali na kuimba Bi Kidude, ni mfanyabiashara ya wanja na hina ambavyo anavitengeneza yeye mwenyewe, pia ni mtaalamu wa matibabu kwa dawa za mitishamba na zaidi ya hayo ni mwalimu mzuri sana wa 'Unyago' na ameanzisha chuo chake mwenyewe na anasema katika wanafunzi wake wote hakuna aliyepata talaka kutoka kwa mumewe.

Bi Kidude amefariki 17 Aprili 2013, Bubu Zanzibar.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!