Thursday 29 April 2021

LITTI KIDANKA MWANAMKE SHUJAA WA SINGIDA ALIYEPAMBANA NA WAJERUMANI KWA KUTUMIA NYUKI

Litti Kidanka ni Mwanamke shujaa wa Singida aliyewaongoza kabila la Wanyaturu katika mapambano dhidi ya utawala wa wakoloni wa kijerumani kati ya mwaka 1903 hadi 1908 .


Litti alizaliwa katika kijiji cha Unyang’ombe , Sekotoure - Ilongero. Aliolewa na Nyalandu Mtinangi Njoka wa Ukoo wa Lundi (antuamwa Lundi) Katika kijiji cha Matumbo Kitongoji Mikuyu, Kata ya Makuro wilayani Singida.
Wazazi wa Litti walikuwa waganga wa tiba asilia baba yake Kidanka Jilu Msasu na mama yake ni Sitra Mughenyi, Litti naye alirithi uganga huo toka kwa wazazi wake.
Ushujaa wake ulijitokeza mwaka 1903 alipoanzisha maasi ya kupinga vitendo viovu vya wakoloni ikiwemo kukamata wapiganaji vijana , kupora ng'ombe na mtama kwa kuwasambaratisha vikali askari wa kijerumani kwa kutumia nyuki wakali waliong'ata walipojaribu kuingia eneo la Wanyaturu .
Maadui wake wakuu, walikuwa ni wakoloni wa Kijerumani waliokuwa wanapora ng'ombe , mtama na kuwakamata watu wenye nguvu kwa ajili ya kuwatumikisha kama watumwa .
Wajerumani walishirikiana na vibaraka wao waliopewa vyeo vya uwakala ambapo eneo la wirwana kibaraka wao wajerumani alikuwa Igwe Yunga wa ukoo wa anyanjoka .
Litti alipambana kuwazuia wajerumani kuingia eneo la wirwana na Mapambano hayo yalichukua miaka mitano kuanzia 1903 yakijulikana kama Maasi ya Litti .
Katika pambano hilo la mara ya pili kati ya wajerumani kikosi cha Litti askari wa kijerumani aliyejulikana kwa jina moja la “SAUSI” aliuwawa kwa kuchomwa mkuki na mume wa shujaa huyo Nyalandu Mtinangi.
Litti alipambana wajerumani mara mbili na kuwashinda. Safari ya tatu mnamo mwaka 1908 Litti hakuweza kufanikiwa kuwashinda, badala yake aliuwawa nyumbani kwake pamoja na mume wake katika kijiji cha Matumbo Kitongoji cha Mikuyu Singida vijijini.
Umaarufu wa Leti ulitokana na ujasiri aliokuwa nao akiwa ni mwanamke, kwa kuwatumia nyuki kama silaha yake ya kuwashambulia maadui huku akisaidiwa na wafuasi wake ambao walikuwa ni mume wake Nyalandu na shemeji yake Hango Linja, wakitumia Mikuki na mishale.
Mwanamke huyo aliongoza mapambano yeye mwenyewe kwa kutoa amri kwa washirika wake kushambulia au kusitisha mapigano katika eneo la vita.
Aidha alijihami kwa kutumia (sumanda) handaki kujificha wasionekane kwa maadui. Hivyo ni baadhi ya vitu vilivyo mjengea umaarufu wa kujulikana katika historia ya mapambano dhidi ya wajerumani.
Anguko la Litti lilitokana na kusalitiwa na wifi yake aliyeitwa Sie Ndinda .
Inaelezwa Sie alirubuniwa na wajerumani ili atoe siri ya ushujaa wa Litti , Igwe Yunga kibaraka wa wajerumani alitumika kumshawishi Sie kwa kuahidiwa ahadi nyingi .
Sie alirudi kwa siri kwenye eneo la zindiko, bila mwenzake kujua alihamisha dawa zote upande wake. Mwenzake Litti alipojaribu kutumia dawa zake alipowaona adui zake wanakaribia zilishindwa kufanya kazi na nyuki hawakuweza kufuata amri Matokeo yake alikutwa nyumbani kwake Mikuyu na kupigwa risasi wakiwa na mume wake na kufariki pale pale. Miili yao ilizikwa baada ya siku tatu, watu walihofia kurudi tena adui zao.
Hapo ukawa mwisho wa mapambano. Wajerumani walikata kichwa cha Litti Kidanka na kuondoka nacho kwenda Kilimatinde na baadae kupelekwa ujerumani .
Litti Kidanka na mumewe Nyalandu Mtinangi walizikwa huko Mikuyu -Matumbo kata ya Makuro na makaburi yao yapo hadi sasa kwakuwa yamewekewa alama ya miti.
Litti alikuwa na watoto wanne, wawili wa kiume na wengine wa kike. Kati yao wakiume ni Sang’ida na Kidanka wasichana ni Nyamughenyi na Sitra.
Watoto wa kike walikamatwa na kuchukuliwa na wajerumani kupelekwa Dar es salaam, baada ya wazazi wao kuuwawa.
Mtoto mwingine aliyeitwa Kidanka, katika purukushani za kuuawa wazazi wao aliweza kuwatoroka wajerumani kwa kuruka uzio na kufyatuliwa risasi alijeruhiwa kwenye ubavu aliweza kukimbia akiwa na jeraha la risasi ubavuni mwake. Kwa kuwa walikuwa na asili ya uganga, naye alipona na kuendelea na shughuli hiyo mpaka alipofariki mwaka 1980 kijijini Matumbo .
Watoto wa kike waliochukuliwa na wajerumani ilikuja kufahamika mmoja aliishi Zanzibar na mwingine aliishi Tabata . Inaelezwa mmoja ya watoto hao wa Litti alimzaa Rais mstaafu wa Tanzania Ally Hassan Mwinyi kwakuwa mwaka 1994 Mwinyi aliwahi kutuma watu kwenda matumbo kufuatilia historia ya bibi yao Litti Kidanka .
Kidanka Mtoto wa Litti aliyewakimbia wajerumani alifanikiwa kupata watoto watano , watatu walifariki na wawili bado wako hai nao ni Msunga Kidanka Nyalandu na Sophia Kidanka Nyalandu , hawa ni wajukuu halisi wa Litti .
Mpaka sasa koo hizi mbili watu wa Lundi na Unyang’ombe hushirikiana kutambika mara kwa mara, katika eneo husika yalipo makaburi ya watu hao, kwa nia ya kunusuru majanga yanayoweza kutokea.
Ni wakati sasa kuhakikisha heshima ya mama huyu inatambulika kama mashujaa wengine mfano Mkwawa na Kinjekitile Ngwale .
Tunao wajibu mkubwa kuhakikisha tunafuatilia fuvu la Litti Kidanka lirejeshwe Tanzania kutoka Ujerumani ili iwe sehemu ya urithi wa historia yetu ya Singida na Tanzania kwa ujumla . Pia ni muhimu kupigania kujengwa makumbusho ya Litti Mkoani Singida .
Maswali na maoni yanakaribishwa .
Rejea / Reffernce
1. Masimulizi ya wazee
2. Kitabu cha mjerumani Von Sick cha mwaka 1916 - Die waniaturu
3. Turu Resistance Movement by Dr. Marguerite Jellicoe 1969 .
Mwisho........



Imeletwa kwenu na Alfred Ringi:

1 comment:

Anonymous said...

Ijengwe shule ya wasichana maeneo hayo ili iwe kumbukumbu kwa shujaa huyu,na historia iweze kuandikwa na kuwekwa wazi juu ya mana huyu

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!