Monday, 29 March 2021

WAGONJWA WA KIFUA KIKUU WAONGEZEKA

 


Kukiwa na ongezeko la kila mwaka la wagonjwa wa kifua kikuu (TB) nchini, Wizara ya Afya imesema hivi sasa inaanza kupata maambukizo mengi ya kifua kikuu sugu kwa wagonjwa wapya.


Kwa mujibu wa takwimu za wizara hiyo, katika miaka mitano iliyopita kumekuwa na ongezeko la kila mwaka tangu 2015 na hivi karibuni wagonjwa wengi wapya wamekutwa na aina hiyo ya juu ya ugonjwa.

Kwa kipindi cha mwaka 2015 wagonjwa wapya waliogundulika walikuwa 62,000, mwaka 2016 (65,908), 2017 (69,623) 2018 (75,845) na mwaka 2019 walikuwa 82,000.

Tatizo hilo limesababisha ugonjwa huo kuwa tishio zaidi kwa kuwa mgonjwa wa kifua kikuu sugu ambaye hajaanza dawa husambaza vimelea hivyo kwa urahisi zaidi.

Miongoni mwa wagonjwa hao ni Elizabeth Ally (25), mkazi wa Manyoni wilayani Singida ambaye alipata tatizo hilo baada ya kuacha matibabu yake ya awali.

“Mwaka 2017 nilipogundulika nilipewa dozi ya dawa za miezi sita nitumie, nilipata changamoto ya kukosa chakula bora, hivyo dawa nilipokuwa nikimeza ziliniumiza sana, nikaacha,” alisema.

Elizabeth alisema baada ya wiki chache alizidiwa na kurudishwa hospitali ambako alianzishiwa dozi ya sindano 60 na dawa nyingine kwa miezi minane na baada ya matibabu hayo alihisi amepona.

“Niliolewa na kupata mtoto wa pili ambaye kwa sasa ana mwaka mmoja na miezi mitatu, lakini Septemba mwaka 2020 nikaanza tena kuumwa, nilipokwenda hospitali nimekutwa na kifua kikuu sugu,” alisema.

Ofisa mpango msaidizi wa mradi wa kifua kikuu Singida, Dk Isabela Nyamizi alisema hali ya kifua kikuu sugu kwa sasa ni changamoto.

“Wagonjwa hawa wanahitaji ufuatiliaji wa karibu, wengi wanakaa maeneo ya mbali na vituo ambako watoa huduma za afya hawajawezeshwa kufika kuhakikisha wanakula inavyotakiwa, wanatumia dawa kwa usahihi na wanaendeleza matibabu, wengine wanakwepa tiba na hicho ndiyo chanzo cha kifua kikuu sugu,” alisema Dk Nyamizi.

Wagonjwa wanaoshindwa kuzingatia utumiaji sahihi wa dawa au kuacha matibabu ndiyo sababu ya vimelea kuzaliana kwa kasi na kujenga usugu wa dawa.

Hali hiyo imetajwa kuwa tishio kwa uchumi wa nchi, kwa kuwa Serikali inatumia Sh11 bilioni kununua dawa na Sh4.6 bilioni kwa ajili ya kununulia vifaa tiba kupambana na kifua kikuu kila mwaka ili kutoa matibabu bure.

Mratibu wa mpango wa taifa wa kudhibiti kifua kikuu na ukoma katika Wizara ya Afya, Dk Allan Tarimo alisema mkoa unaoongoza kwa TB hiyo ni Dar es Salaam ambako asilimia 20 ya wagonjwa wapya wanatokea.

Mikoa mingine ni Mbeya, Arusha, Geita na Manyara, huku akiitaja mikoa yenye wagonjwa wachache zaidi kuwa ni Kigoma, Katavi, Songwe, Unguja na Pemba.

Dk Tarimo alisema uwezekano wa kupata kifua kikuu kutoka kwa mtu unayeishi au kufanya kazi naye ni mkubwa kuliko kutoka kwa mgeni na kwamba aliyeanza kutumia dawa angalau kwa wiki mbili haambukizi.

Alizitaja dalili za kifua kikuu kuwa ni kukohoa, wakati mwingine kukiwa na makohozi ya damu, kuhisi baridi, uchovu, homa, kukonda kwa mwili, kukosa hamu ya kula na kutoa jasho jingi isivyo kawaida hasa nyakati za usiku.

“TB huathiri hasa mapafu, lakini inaweza kuathiri vilevile sehemu nyingine za mwili na dalili zinaweza kubadilika. Bila kupata tiba huweza kusambaa kwenye sehemu nyingine za mwili kupitia mfumo wa damu.

“Ikishambulia mifupa inaweza kuleta maumivu ya uti wa mgongo na kuharibu maungio ya mifupa, ikishambulia ubongo husababisha meningitis, ikienda kwenye maini na figo huweza kusababisha damu ndani ya mkojo na ikishambulia moyo inaweza kuathiri uwezo wa moyo wa kusukuma damu na inaweza kusababisha kifo,” alisema Dk Tarimo.

Dk Tarimo alisema makundi yaliyo hatarini kuugua kifua kikuu ni pamoja na watu wenye virusi vya Ukimwi, watoto chini ya miaka mitano, wenye utapiamlo na tatizo la lishe, magonjwa sugu ikiwamo saratani, kisukari, wanafunzi wa shule za bweni, wachimbaji migodini na magerezani.

Hata hivyo, alisema kinga ya magonjwa hayo ni kuepuka misongamano isiyo ya lazima. “Tunashauri mtu unapopiga chafya ujizuie na kitambaa, kuepuka maeneo yenye msongamano na pia tunasisitiza watoto wapate chanjo ya kukinga kifua kikuu ili hata ikitokea akapata basi haitakuwa kali kwake.”

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!