Sunday 12 January 2020

MBINU 11 ZA KUPUNGUZA UZITO NA UNENE BILA ZOEZI


Kuendelea kutegemea mazoezi au kufunga kula au kupunguza kula kunaweza kusiwe msaada kwa baadhi ya wengine wanaotaka kupunguza uzito na unene wa miili yao.

Hata hivyo zipo mbinu chache unazoweza kuzitumia na ukaweza kudhibiti uzito wako.
Bila kukupigisha stori nyingi hapa chini nakuelezea mbinu hizo bila kuchelewa kama ifuatavyo:
Mbinu 11 za kupunguza uzito na unene bila mazoezi wala kufunga kula
1. Kula chakula pole pole
Ubongo wako unahitaji muda wa kutosha kushughulika na hilo tendo la kutafuna na kumeza chakula.
Kula pole pole kunahusiana moja kwa moja na kuweza kula chakula kichache na kujisikia kushiba.
Ni muda gani unatumia kumaliza chakula chako unaweza kuathiri pia uzito wako.
Utafiti unaonyesha watu wanaokula kwa haraka haraka hutokewa kuwa na uzito mkubwa pia ukilinganisha na wale wanaokula pole pole.
Jaribu hii haitakugharimu kitu.
2. Tumia sahani ndogo kwa vyakula visivyo na afya
Kama itakutokea ukataka kula vyakula visivyo na afya ambavyo huongeza uzito kirahisi basi jaribu kutumia sahani ndogo na siyo unayotumia kila siku. Mara nyingi watu wengi chakula kinapoisha kwenye sahani hujiona tayari inatosha.
Hivyo sahani ndogo inakifanya chakula kionekane kingi na kikubwa na hivyo kuridhisha macho na njaa yako kwa ujumla.
Kazi inabaki kuwa kwako mara zote.
3. Kula zaidi protini
Vyakula vyenye protini vina matokeo makubwa upande wa njaa. Vyakula hivi vinakufanya ujisikie umeshiba kwa kipindi kirefu kama ilivyo kwa vyakula vyenye nyuzinyuzi.
Kama kwa sasa asubuhi unakula chakula cha asubuhi chenye wanga mwingi kama mikate, chapati au maandazi au hata wali basi unaweza kuhamia kula vyakula vyenye protini nyingi kama vile mayai.
Vyakula vingine vyenye protini nyingi ni pamoja na korosho, samaki, mtindi, parachichi, karanga, mbegu za maboga, nk nk
4. Weka mbali vyakula visivyo na afya
Vyakula vile unavyofahamu kwa hakika kwamba huongeza uzito na unene kirahisi ni vema ukavihifadhi mbali na macho yako hivyo hutashawishika kutaka kuvila.
Hili nalo ni rahisi kulitekeleza na kazi inaendelea kuwa kwako tu.
5. Kula zaidi vyakula vyenye nyuzinyuzi
Vyakula vyenye nyuzinyuzi (faiba) vinao uwezo wa kukufanya ujisikie umeshiba kwa muda mrefu.
Vyakula hivi mara nyingi hutokana na mimea hasa maharage, machungwa, parachichi, mbegu za maboga, karoti, mayai, ndizi, nk
6. Acha kukaa kwenye kiti masaa mengi
Umewahi kujaribu kufanya mazoezi, kubadili chakula au hata kufunga na bado ukawa unasumbuliwa na kitambi au uzito kuwa mkubwa? Basi jibu la tatizo lako ni kukaa kwenye kiti masaa mengi.
Utafiti unaonyesha kukaa tu kwenye kiti hata kama hauli chakula kingi bado utaendelea kuongezeka uzito.
Kwahiyo kama unataka kuondoa kitambi au tumbo au kupungua uzito kwa haraka acha kukaa masaa mengi kwenye kiti, hata kama kazi yako ni ya ofisini jaribu namna unaweza kupata meza ya kusimama huku unaendelea na kazi yako.
7. Pakuwa vyakula visivyo na afya kwenye sahani nyekundu
Mbinu hii ya kushangaza ni kuwa unachohitaji kufanya ni kuweka chakula ambacho si afya yaani vile vinavyoongeza uzito kama chipsi, maandazi na vingine kama hivyo katika sahani ambayo ni nyekundu .
Utafiti mmoja ulionyesha kuwa watu walifanikiwa kula chakula kidogo baada ya kuwa wanawekewa chakula kwenye sahani nyekundu ukilinganisha na wakati walipowekewa kwenye sahani za rangi nyingine.
Maelezo ni kuwa mara nyingi tunahusianisha rangi nyekundu na alama ya kusimama na maonyo mengine katika maisha yetu ya kila siku.
8. Acha vinywaji vyenye sukari sana
Viongeza utamu vya kutengenezwa (artificial sweetners) na sukari kwa ujumla vimekuwa vikiwekwa kwenye vinywaji vingi miaka ya sasa.
Vinywaji vyenye sukari kama soda vimekuwa vikihusishwa na kuongezeka kwa mwili moja kwa moja.
Ni rahisi zaidi kuongezeka uzito ukitumia vinywaji hivi kwakuwa nishati yake ni rahisi kubebeka na kuvumilika tofauti na ile ya kwenye vyakula vigumu.
Kukaa mbali na vinywaji hivi na juisi nyingine zozote za dukani na hata za nyumbani zenye sukari ni namna nzuri ya kudhibiti uzito bila kuhitaji mazoezi wala kufunga kula.
Badala yake kunywa zaidi zaidi maji au chai ya kijani (green tea) au chai ya viungo mbalimbali (spiced tea) ukitumia asali kwa mbali badala ya sukari.
9. Pata usingizi mzuri na epuka msongo wa mawazo
Linapokuja suala la kuwa na afya bora kupata usingizi mzuri na kutokuwa na msongo wa mawazo (stress) ni vitu viwili haviepukwi. Usingizi na sress vyote viwili vinaweza kuwa na matokeo ya moja kwa moja kuhusu njaa na uzito wako.
Ukosefu wa usingizi mzuri kunaweza kuzisababishia homoni zinazohusika na kuweka sawa njaa (leptin na ghrelin) kutokufanya kazi zake vizuri. Homoni nyingine iitwayo “cortisol” ambayo inahusika na utulivu pia inakuwa imeongezeka sana wakati unapokuwa na msongo wa mawazo.
Homoni hizi zikiwa zimesumbuliwa hivyo kiasi chako cha njaa kitaongezeka pia uhitaji wako wa kula vyakula visivyo na afya utaongezeka mara dufu.
Kile ulikuwa hujuwi ni kuwa kama hupati usingizi mzuri na wa kutosha unakuwa na uwezekano mkubwa wa kupatwa na ugonjwa wa kisukari aina ya pili.
10. Wakati unakula usitumie simu au kompyuta
Kuwa makini na akili yote ukiiweka katika chakula tu kunaweza kusaidia kula kidogo.
Watu ambao wanakula huku wanatumia simu, kompyuta au wanaangalia luninga (TV) au wanacheza gemu huwa wanakula chakula kingi bila wao kujua.
11. Kunywa maji mara kwa mara
Kunywa maji mara kwa mara kunaweza kukusaidia kula chakula kidogo na hivyo kupunguza uzito hasa kama utakunywa nusu saa au robo saa kabla ya chakula.
Kunywa nusu lita nusu saa kabla ya chakula na utaona umefanikiwa kula chakula kidogo na hivyo utaweza kupungua uzito kirahisi.
Hutakawia kuona faida ya mbinu hii kama utakuwa umeamua kila siku kunywa maji kila mara na zaidi kila nusu saa kabla ya chakula

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!