Sunday 12 January 2020

BURIANI SULTAN QABOOS, MAISHA YAKO NI CHUO CHA MAFUNZO.



Na Ismaili Mussa (Mchambuzi wa Masuala ya Siasa na Uongozi) - 0765747174.
Siku ya Jumamosi Januari 11, dunia inaanza Safari rasmi ya kumsahau Mfalme Qaboos bin Said Alsaid kwa kuiacha Omani aliyeipatia karibu kila hadhi na sasa anakwenda kuhifadhiwa katika katika tumbo la ardhi. Sultan Qaboos alizaliwa Novemba 18, 1940 akiwa mtoto wa kiume pekee wa familia ya mfalme wa Omani huku kukiwa kumekolea joto la mapigano ya Vita kuu ya pili ya dunia: ingekuwa huku Afrika mashariki haswa pwani angeitwa Mvita au Vita.

Jemedari huyu aliyepambana vita baridi na mzazi wake; alizaliwa katika eneo la Salalah, Muscut - Oman na Baba yake aliitwa Said Bin Tamur aliyekuwa mfalme wa Omani na mama yake aliitwa Sheikha Mazoom Al - Mashani ambaye inadaiwa ana nasaba na Tanzania katika Visiwa vya Zanzibar ambavyo vimewahi tawaliwa na Omani baada ya Sultan Seyyid Said ambaye alihamishia makao makuu ya nchi kutoka Muscut hadi kuwa Zanzibar, Unguja eneo la Stonetown.
Sultan Qaboos alikuwa Muumini wa dini ya Uislam wa madhihabu ya Ibadi. Alianza elimu yake ya Msingi na kisha kuendelea na elimu ya sekondari akiwa Katika eneo alozaliwa la Salalah bila kukosa elimu ya dini ya Kiislamu, kisha akapelekwa Bury - St. Edmunds Uingereza akiwa na miaka 16 kuendelea na masomo akiwa na umri wa miaka 20 alijiunga chuo cha kijeshi kilichoitwa Royal Military Academy Sandhurst cha nchini Uingereza na kumaliza mwaka 1962, kisha akajiunga na jeshi la Uingeza na kupangiwa Vita ya Wakameruni na kufanya kazi Ujerumani kwa mwaka mmoja.
Baada ya jeshi Qaboos alijiunga na masomo ya serikali za mitaa akiwa Uingereza na kukamilisha elimu yake kwa kufanya Safari ya aliyochaguliwa Kama mchezaji wa mpira wa kikapu.
Mwaka 1966 Sultan Qaboos akiwa bado mtoto wa mfalme anarejea kwa mtazamo wa mlango wa sita wa fahamu usiotumiwa na wengi anaonekana ni jasusi aliyebobea, anafika nyumbani inadhihirika msemo wa masikio hayavuki kichwa Qaboos anawekwa kizuizini katika Kasri la kifalme la baba yake mzazi na baba yake mwenyewe na kuzuiwa katakata asijihusishe na masuala ya michakato ya mipango ya maendeleo ikiwa Marehemu Qaboos anapata hamu ya kufanya mabadiliko ambayo baadae yaliratibiwa kwa msaada wa Wafanyakazi wa Kigeni, Taasisi ya kijasusi ya Uingereza ya M16, Watumishi wa Wizara ya Ulinzi na mambo ya nje ikiwa imeidhinishwa na Waziri Mkuu wa wakati huo aliyeitwa Harold Wilson. Vuguvugu hili la baba na Mwana linafikia tamati 23 Julai ya 1970 kwa Mwana kumpindua Baba yake kwa Vita baridi kwa msaada wa karibu wa nchi ya Uingereza na kuanza kuitawala Omani kwa kuibadili jina na kuiita 'Oman Sultanate', kwa kweli hili ni jambo la aina yake katika dunia hii kwa kumpindua baba yake Mzazi katika madaraka, huenda wengine tendo hili wangetafsiri kama kuwa ukosefu wa adabu kwa Qaboos dhidi ya Baba yake na kwa lugha ya Sasa tungesema; amekaribia kuanza ile biashara isiyo na staha ya kuokota machupa au makopo, lakini wapi! Sultan Qaboos anaupindua utawala wa baba yake ambaye vyanzo vinaonyesha alikuwa na utawala wa kibabe na kimabavu kufikia hatua ya kukataza kumiliki luninga na miwani, nchi ilitawaliwa na Uvunjaji wa haki za binadamu pamoja na biashara ya utumwa, Basi tena Qaboos anakuwa Mfalme wa Omani na kuanzisha sera za kimamboleo na maendeleo, alisitisha kujitenga kwa Omani na masuala ya Kimataifa, akakomesha utumwa, ikawa Mwisho wa Uasi wa dhofar na kutanganzwa kwa katiba ya Omani.
Marehemu Qaboos akachukua nchi ikiwa masikini ya kutupwa, haina miundombinu ya afya, elimu, barabara ilikuwa maili 6 iliyowekwa lami huku kundi kubwa la Waomani maisha yao yakitegemea Kilimo na Uvuvi. Qaboos anaanzisha mambo mapya na ya kisasa kwa kutumia mapato ya mafuta, alijenga shule, hospitali, miundominu ya barabara mpya zilizowekwa lami, mawasiliano ya simu na kimtandao, bandari, viwanja vya ndege, vyanzo vipya vya maji, na kuweka mazingira rafiki ya biashara kwa kuanzishwa kwa mabenki, hoteli, makampuni ya bima, uchapaji yakaanza kuonyesha nchi inakuwa kiuchumi. Ikaanzisha sarafu yao iliyoitwa Rial ya Omani na kuikacha Rupia ya India iliyokuwa inatumika awali. Vyuo Vikuu vikafunguliwa, akaruhusu watu wa imani nyingine wawe na uhuru wa Kuabudu hadi kufikia hatua ya kujitolea kufadhili ujenzi wa makanisa manne ya Kikatoliki na Kiprotestanti na dhehebu la Kihindu kwa ajili ya kuabudu, utawala wake Sultan Qaboos Bin Said ukajidhihisha kuwa ni utawala kamili (Absolute Monarch). 
Mnamo Tarehe 22 Machi 1979 Qaboy Bin Said alifunga ndoa na kuuacha ubarobaro na binamu yake aliyeitwa Kamli Sayyida Nawwal binti Tariq Alsaid aliyezaliwa 1951 akiwa binti wa Sayyid Tariq Bin Taimur Alsaid ambapo ndoa hii ilidumu takribani miaka mitatu hadi kufikia 1979 waliachana japo haikuwekwa wazi sababu ha kuachana kwao na hawakuwa wamepata mtoto, inasimuliwa kuwa mfalme hakuoa tena mpaka mwaka 2005 akiwa na Umri wa miaka 65 Mfalme alipoamua kuoa tena na akamuoa Sayyida Shawana Bint Nasir Alsaid ambaye hadi anafariki Hakuwa nae na hawakufanikiwa kupata mtoto.

Mambo yanayovuta hisia katika historia ya Omani yanayofungamana na Mfalme Qaboos ni ile siku ya mapinduzi Julai 23 huchukuliwa Kama siku ya kuzaliwa upya kwa taifa lao (Uhuru) na cha kufurahisha ni kuwa Waomani huungana na Mfalme ifikapo Novemba 18 ya kila mwaka siku ya kuzaliwa kwake ambayo huwa Sikukuu (Mapumziko) ya Kitaifa.
Omani haina mfumo wa mihimili ya serikali (Separation of power) Kama mfano ilivyo nchini kwetu Bunge, Mahakama Baraza la Waziri ambayo huruhusu ufuatitiaji na Usawazishaji (Check and balance), madaraka yote anakuwa nayo Sultani ambaye ndio Amiri jeshi Mkuu, Waziri wa Mambo ya ndani, Mambo ya nje na M/kiti wa benki Kuu.
Maisha binafsi ya Sultan yameghubikwa na maswali mengi Kama Vile; kwanini hakuwa na mtoto japo inafahamika watoto ni majaliwa yake maulana lakini ufalme na sifa zake za uongozi bora zilikuwa zinawasukuma kuona Kama haitendei haki jamii yake kwa kukosa warithi wa kutoka katika damu yake, kwanini alikaa katika ndoa kwa muda mfupi au ndio hakuna mbabe wa mapenzi maana kitendo cha mfalme kuachana na aliyekuwa mkewe mwaka 1979 hadi aje kuoa mwaka 2005 na kisha kutodumu nae nacho kinazua maswali ya udadisi kutaka kufahamu kulikoni? Kuna simulizi zisozo rasmi kuwa mfalme alikula kiapo cha kutotaka kupata mtoto kwa kuwa akihofia swala zima la urithi wa kitabia za kibaolojia (The genetics) ambapo ingewezekana angepata mtoto au watoto ambao wenye urithi wa damu ya kikatili wa babu yao na kuichafua Omani ambayo yeye ameshiriki kuijenga kwa Jasho na damu. Huenda fununu hii ikawa na ukweli kwa kuwa hakupenda damu yake irithi kiti chake cha ufalme na kufikia hatua ya kuandika barua ya siri ya mrithi wake ambaye ni mtoto wa mjomba wake aitwaye Haitham Bin Tariq Alsaid na kuuhamisha ufalme upande wa baba yake, katika nchi za falme za kiarabu ni Oman pekee ndio utaratibu wa mrithi wake haukutangazwa kwa Umma kabla ya kifo cha mfalme.

Mfalme Qaboos katika maisha yake amewahi kupata ajali ya gari nje ya kasri huku ikimgharimu maisha ya Waziri wake nguli na muhimu Bwana Qais Bin Abdul Munim Al Zawawi. Kifo chake kimekuwa cha kusisimua na kuvuta hisia karibu maeneo mengi ya dunia huku raia wake waikitaja kuwa wamepoteza shujaaa aliyekuwa mfano wa kiongozi bora kwa kuwa aligusa maisha yao lakini pia hata kwa watu waliowahi fika au kuishi Omani wanamsifu na kumtaja kama kiongozi aliyekuwa aliyewajali raia wake.
Jabari hili la siasa na mwanadiplomasia mashuhuri wa siasa za Mashariki ya Kati, tamati ya maisha yake yamekalishwa na ugonjwa wa saratani ambapo mwaka 2019 ilimfikisha nchini Ubeligiji kutibiwa lakini haikufua dafu hatimaye Januari 10, 2020 sawa Jamadul -Awali, mwezi 14, 1441 kwa kalenda ya Hijiria roho yake imetwaliwa na Mwili wake kuhifadhiwa katika makaburi ya familia ya ghala baada ya swala ya jeneza iliyofanyika katika msikiti mkubwa wa Alghubura.
Hakika Dunia ina Kila aina ya watu ambao hutengeneza Visa na Mikasa
Innalirah waina illaih rajiun.
Wasalam
©Ismaili Mussa (Mchambuzi wa Masuala ya Siasa na Utawala)
Dodoma - Tanzania.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!